................
Na Daniel Limbe,Biharamulo
KATIKA kile kilichoonekana ni kuitukuza, kuithamini na kuiendeleza lugha adhimu ya Kiswahili hapa nchini, madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera,wamegomea uwasilishwaji wa elimu ya chakula na lishe baada ya kupelekwa kwenye kikao chao kwa lugha ya kiingereza.
Ni baada ya Ofisa lishe wa wilaya hiyo,Domina Jeremia,kutaka kuwasilisha elimu hiyo kwa njia ya kifaa cha kukuzia picha na maandishi(Projector machine) huku maandishi hayo yakisomeka kwa lugha ya kiingereza licha ya kufanya tafsiri kwa lugha ya kiswahili.
Kabla ya uwasilishaji huo,baadhi ya madiwani hao akiwemo wa viti maalum, Ziyun Husseni na diwani kata ya Nyakahura,Apolinary Mugarula,waliohoji sababu ya kutumia lugha ya kiingereza badala ya kiswahili ambayo ndiyo lugha mama ya taifa la Tanzania.
Diwani wa Kata ya Biharamulo mjini, David Mwenenkundwa alitaka kufahamu sababu za kutoiheshimu lugha ya taifa katika uwasilishaji wa taarifa mbalimbali za serikali ikiwemo vikao halali vya madiwani badala yake kuamua kutukuza lugha ya kutoka nchi za ng'ambo.
" Hivi ni kwanini muwasilishaji wa elimu hii alete kwetu kwa lugha ya kiingereza badala ya kiswahili,kuna sababu gani zilizomsababisha ashindwe kuitafsiri kwa kiswahili ili tuwe na uelewa wa pamoja badala yake atumie lugha ya kutoka ng'ambo"amehoji Mwenenkundwa.
Akijibu malalamiko hayo,Ofisa lishe huyo amesema hali hiyo imetokana na udharura wa kuandaa na kuipeleka taarifa hiyo mkoani haraka kwa siku ya kesho na kwamba muda usingetosha kuandaa taarifa nyingine kwa lugha ya kiswahili.
Baada ya kauli hiyo baadhi ya madiwani hao wameonekana kuipinga vikali kwa madai ripoti hiyo ilipaswa kuandaliwa mapema kwa lugha ya kiswahili ili kuwajengea uelewa wa pamoja madiwani hao badala ya kisingizio cha ripoti hiyo kuhitajika mkoani Kagera.
Kutokana na mjadala huo,mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu, akalazimika kuagiza taarifa hiyo irudishwe na kuandaliwa upya kwa lugha ya kiswahili ili kesho kabla ya kikao cha Baraza la madiwani kuendelea iwasilishwe ili kujua hali halisi ya chakula na lishe kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja waataifa la elimu,Sayansi na Utamaduni(UNESCO) Novemba 23,2021 lilitangaza rasmi kuwa kila mwaka Julai 7 itakuwa siku ya Kiswahili duniani.
UNESCO ilipitisha uamuzi huo huko makao makuu yake mjini Paris Ufaransa wakati wa mkutano wa nchi wanachama wa shirika hilo na utekelezaji wake ukaanza kutumika mwaka 2022.
Post a Comment