PGI SOLUTION YAZINDUA PUNGUZO APP KWA BEI NAFUU KUPITIA MPESA

Kampuni ya PGI Solution Limited imezindua programu mpya ya kibunifu iitwayo Punguzo App, ambayo inatoa fursa kwa Watanzania kununua bidhaa mbalimbali kwa punguzo kubwa la bei kupitia Mpesa Super App ya Vodacom.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa PGI Solution Limited, Gillsant Mlaseko, alifafanua kuwa Punguzo App ni suluhisho la kipekee linalowezesha Watanzania kupata bidhaa za kila aina kwa bei nafuu kwa kutumia Mpesa, na kwa kushirikiana na Vodacom, programu hii inalenga kuwafaidi wateja kwa kuwaletea punguzo kwenye bidhaa kama vifaa vya kielektroniki, mitindo, vipodozi, na bidhaa za nyumbani.

"Kwa wateja wa Mpesa, Punguzo App inawawezesha kununua bidhaa kwa urahisi kupitia app ya Mpesa Super na kuwa na chaguo la kuchukua bidhaa moja kwa moja dukani au kuzipokea kwa njia ya usafirishaji hadi walipo," alisema Mlaseko. 

Aliongeza kuwa huduma hii inatoa fursa kwa wafanyabiashara kuunganishwa na wateja wapya kwa urahisi, na hivyo kuongeza mauzo yao kupitia jukwaa linalotumiwa na Watanzania wengi.

Katika hatua nyingine, Meneja wa Malipo ya Mtandao na Mifumo ya Kidijitali Vodacom Mpesa, Josephine Mushi, alieleza kuwa Punguzo App inalenga kuboresha uzoefu wa ununuzi kwa wateja wa Mpesa, kwa kuwapa fursa ya kununua bidhaa kwa bei nafuu. 

Alisema kuwa Vodacom inaendelea kuunga mkono juhudi za kuleta bidhaa bora kwa bei nafuu na kwamba wateja wa Mpesa wanahamasishwa kutumia Punguzo App ili kufurahia ununuzi wa bidhaa, hasa katika kipindi cha sikukuu ya Krismasi.

"App hii itawafaidi wateja wetu kwa kutoa bidhaa bora kwa bei nafuu, na tunatoa wito kwa Watanzania kutumia fursa hii, hasa katika kipindi cha Krismasi ambapo wengi wanapeana zawadi," alisema Mushi.

Kwa kutumia Punguzo App, Watanzania sasa wana fursa ya kununua bidhaa bora kwa urahisi na bei nafuu, huku wafanyabiashara pia wakinufaika kwa kuweza kuunganishwa na wateja wapya kupitia platform hii ya kidijitali.

 

 

 

 

 


 

0/Post a Comment/Comments