*******
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameiona haja ya kuongeza muda zaidi wa uokoaji wa watu waliofukiwa na kifusi cha ghorofa lililoanguka hivi karibuni Kariakoo jijini Dar es Salaam, kutoka saa 72 hadi saa 96.
Novemba 19,2024 Rais Samia amempigia simu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kumtaka kuongeza saa 24 zaidi kutoka zile 72 za awali ili kuwaokoa watu wanaodhaniwa kuwa bado wapo chini ya jengo hilo.
"Mheshimiwa Waziri Mkuu ninatambua utaratibu wa uokoaji una muda maalum wa saa 72 mpaka kusitisha zoezi hilo, binafsi nina matumaini kuwa Mwenyezi Mungu anaweza akatenda miujiza yake na kuweza kuwanusuru ndugu zetu wengine ambao bado wamenasa kwenye jengo hilo.
"Ninakupa maelekezo ya kutositisha zoezi la uokoaji na kuongeza muda wa saa 24 zaidi ili kuwapambania ndugu zetu ambao tunaamini bado wako hai."
Aidha Rais Samia ameonesha kutambua na kutathimini mchango mkubwa wa uokoaji unaofanywa na vikosi vyote na wananchi kwa ujumla ambao kwa pamoja wanashiriki katika zoezi hilo.
"Nina wathamini sana, wameonesha utu, uzalendo mkubwa na uchapakazi wa hali ya juu sana, hivyo nawatia moyo na kuwapa nguvu ya kuendelea kuwapambania ndugu zetu kwani ninyi ni mashujaa wa taifa letu."
Rais Samia amewasihi wananchi, ndugu na jamaa kuwa na subira na kama taifa tuendelee kuwaombea ndugu zetu na wapiganaji wetu ili kufanikisha zoezi hilo kwa mafanikio makubwa.
Post a Comment