RAIS SAMIA MGENI RASMI KONGAMANO LA SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UBUNIFU



Na Okuly Julius Dodoma


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. SAMIA SULUHU HASSAN anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Tisa la Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu linalofanyika kila mwaka chini ya uratibu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).

Kongamano hilo, litafanyika kuanzia tarehe 2 hadi 4 Disemba, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.

Waziri Wa Elimu, Sayansi Na Teknolojia, Profesa ADOLF MKENDA akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya Kongamano hilo Jijini Dodoma amesema linalenga kuwaleta pamoja watafiti, wabunifu, na wadau kutoka sekta mbalimbali, ndani na nje ya nchi ili kujadili kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha mchango wa Sayansi, teknolojia na ubunifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Amesema kupitia Kongamano hilo Serikali itapata michango ya kisera na kitaalamu ambayo itasaidia kuimarisha sera, mikakati, na juhudi nyingine zinazolenga kuimarisha mchango na mshikamano baina ya taasisi, sekta binafsi, na wadau wa maendeleo katika kuendeleza Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kama nyenzo kuu ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya watanzania.

Pamojana na masuala mengine Rais Dkt.Samia atazindua rasmi mfuko wa mikopo kwa ajili ya kusaidia bunifu na teknolojia zinazobuniwa na vijana wa Kitanzania, atakabidhi hundi ya Shilingi bilioni 6.3 kwa watafiti 19 na atawatambua na kutoa tuzo maalumu kwa wanasayansi na wabunifuambao matokeo ya kazi zao yamechangia kuleta mabadiliko ya kiuhumi na kijamii, ndani na nje ya nchi.

"ili kufanikisha na kufikia malengo yaliyokusudiwa, nitumie fursa hii kuwaalika Watanzania wote pamoja na wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi, ndani na nje ya nchi, kushiriki Kongamano hili la STICE,"

Na kuongeza kuwa "Ushiriki wenu ni muhimu sana katika kuleta mawazo na mikakati mipya, kuimarisha utafiti na ubunifu, na kuhakikisha kuwa matokeo ya utafiti na ubunifu yanajibu mahitaji na kutatua changamoto za maendeleo ya kiuchumi na kijamii,"

Kauli mbiu ya Kongamano kwa mwaka huu ni "Matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ununifu katika Kuhimili Changamoto za Mabadiliko ya Tabianchi na Kuchangia kwenye Uchumi Shindani”.





0/Post a Comment/Comments