📌 *Lengo ni kuimarisha upatikanaji wa umeme*
📌 *Fidia kulipwa kwa wanaopisha mradi*
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema Serikali inatekeleza mradi wa kuiunganisha Mikoa ya Mtwara na Lindi na umeme wa gridi kutokea Songea kwa kupitia njia ya Tunduru, Masasi -Mahumbika.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Novemba 04, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Zuberi Kuchauka, Mbunge wa Liwale aliyetaka kufahamu uamuzi wa Serikali kuhusu ujenzi wa kituo cha umeme Jimbo la Liwale.
"Umuhimu wa kujenga kituo cha umeme Liwale upo kwa sababu kitaboresha upatikanaji wa umeme Liwale, nimhakikishie Mhe. Mbunge kwa sasa tunatekeleza mradi mkubwa wa kupeleka umeme wa gridi ya Taifa kwa mikoa tajwa." Amesema Mhe. Kapinga
Akijibu swali la Mbunge wa Namtumbo, Mhe. Victor Kawawa aliyetaka kufahamu ni lini wananchi waliopisha mradi wa gridi ya Taifa kwenda Mikoa ya Mtwara na Lindi watalipwa fidia, Mhe.Kapinga amesema agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha wananchi hao wanalipwa fidia linatekelezwa.
Kapinga, ametoa rai kwa wananchi hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa kupisha maeneo yao ili mradi uweze kukamilika kwa wakati kwa manufaa ya Taifa.
Akijibu swali la Mbunge wa Meatu, Mhe. Leah Komanya aliyeuliza Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme katika Wilaya ya Meatu, Mhe. Kapinga amesema Wilaya ya Meatu inapata umeme kutokea Kituo cha Kupoza umeme cha Ibadakuli kilichopo Mkoani Shinyanga umbali wa kilomita 135.
Aidha, kukatika kwa umeme wilayani Meatu kunatokana na umbali mrefu wa njia ya kusafirisha umeme pamoja na uchakavu wa miundombinu ya umeme.
Mhe. Kapinga ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kufungwa vidhibiti umeme katika njia ya awali, kujenga njia ya kusafirisha umeme kutoka Mkalama Mkoani Singida hadi Bukundi Wilayani Meatu pamoja na zoezi la kubadilisha nguzo zilizochakaa kwa kuweka nguzo za zege.
"Mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imeanza kutekeleza ujenzi wa Kituo cha kupoza umeme katika eneo la Imalilo, Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu ambapo itajengwa line ya umeme kutokea kwenye kituo hicho hadi Meatu." Amesisitiza Mhe.Kapinga.
Akijibu swali la Mbunge wa Bunda Mjini, Mhe. Robert Chacha aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itakamilisha usambazaji wa umeme kwenye mitaa ya Halmashauri ya Mji wa Bunda, Mhe. Kapinga amesema tayari Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa vitongoji kumi na tano.
Akijibu swali la Mbunge wa Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Waitara aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itakamilisha usambazaji wa umeme katika Jimbo la Tarime Vijijini, Mhe. Kapinga amesema tayari Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa vitongoji kumi na tano.
Ameongeza kuwa kuanzia mwezi Desemba mwaka huu Serikali itaanza kutekeleza mradi mwingine wa Vitongoji 4,000 nchini.
Post a Comment