******
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry William Silaa (Mb) amesema kuwa kutokana na kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), serikali inaendelea kudhibiti usalama mtandao nchini ili kuhakikisha uhalifu unaofanyika kupitia mitandao unakomeshwa.
Waziri Silaa ameyasema hayo akiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mhandisi Hamad Masauni (Mb), katika kikao kilichowakutanisha waatalamu wa wizara hizo mbili, wadau wa usalama mtandao pamoja na Watoa Huduma za Mawasiliano Nchini kilichofanyika leo tarehe 22 Novemba, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) jijini Dar es Salaam.
“Sisi kama wizara hatuwezi kukaa kimya, lazima tufanye jitihada za kudhibiti hali hii, hivyo tukaona ni muhimu tukutane pamoja ili tujadiliane njia bora zaidi ambayo itasaidia kuondokana na changamoto hii, serikali inachukizwa na kuona watanzania ambao watajitafutia kipato chao kwa jasho lakini wengine wanafanya uhalifu wa kuweza kuiba kipato chao, tuna nia ya dhati ya kuhakikisha jambo hili linafanyiwa kazi ya kuhakikisha tunakomesha jambo hili na kuhakikisha tunasimamia wananchi ili kuondokana na jambo hili.” Amesema Waziri Silaa.
Amesema Tanzania ni moja kati ya nchi zinazofanya vizuri duniani katika kusimamia masuala ya usalama wa mtandao ambayo ni kazi kubwa inayofanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) lakini wahalifu nao wanatafuta mbinu mpya kila siku.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mhandisi Hamad Masauni (Mb) wakati akisoma maazimio ya kikao hicho amesema uhalifu wa mtandao ni suala mtambuka na linagusa sekta ya umma na binafsi hivyo ni wajibu wa sekta hizo kuhakikisha kila mmoja anatimiza majukumu yake kwa weledi.
“Ni imani yetu tuliyojadiliana tunaenda kuyatekeleza ili kuweza kusaidia kulipunguza tatizo hili la uhalifu wa mitandao, uhalifu wa mtandao ni suala mtambuka na linagusa sekta ya umma na binafsi, ni wajibu wetu kuhakikisha kila mmoja anatimiza majukumu yake kwa weledi, kwa upande wa wizara yangu namshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya ya uwezekaji ndani ya wizara, ya kuimarisha vitendea kazi, vifaa vya TEHAMA kwenye maeneo mengi ikiwepo maeneo ya usalama wa mitandao na kukiongezea uwezo kitengo hicho” amesema Mhe. Masauni.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabir Bakari Kuwe amesema ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano duniani kote umechangia kasi ya ukuaji wa uchumi wa kidigitali ambapo kwa nchini Tanzania hadi kufikia mwezi Septemba, kulikuwa na laini za simu milioni 80.7, watumiaji wa mtandao wa intaneti milioni 41.4 ambapo ukuaji huo umekuja na changamoto zake ambazo ni za dunia nzima.
“Unajua teknolojia inavyokuwa inaleta mambo mengi mazuri, lakini pia inaleta uwezekano wa watu ambao sio wazuri kufanya uhalifu, zipo aina tofauti tofauti za uhalifu zingine zinatumia teknolojia, yaani wahalifu wanakua wanajua sasa hivi wastaafu watakuwa wamepokea mafao, sasa hivi mawakala watakuwa na hela, kwa hiyo wanatafuta njia ya uhalifu kupitia mtandao hivyo tunahitaji kuimarisha madawati ya huduma na tukashirikiana” amesema Dkt. Jabir.
Post a Comment