Na mwandishi wa Dar es salaam,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, ameziagiza taasisi za umma kuhakikisha zinatekeleza sheria ya usalama na afya mahali pa kazi ili kulinda nguvu kazi ya Taifa na kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi.
Akizungumza katika
ziara yake aliyoifanya katika Ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi
(OSHA) mnamo Novemba 16, 2024, katika kuhitimisha zoezi la ukaguzi wa mifumo ya
Utumishi wa Umma uliofanyika kwa taasisi za serikali zipatazo 160 Mhe.
Simbachawene amesema moja ya vipengele kati ya vipengele 13 ambavyo tume ya
Utumishi wa Umma iliyokuwa inakagua ni Pamoja na na utekelezaji wa sheria na kanuni zinazohusiana
na usalama na afya mahali pa kazi.
“Sote tunafahamu kuwa kinga ni bora kuliko tiba. Sheria ya
Afya na Usalama Mahali pa Kazi Na. 5 ya Mwaka 2003 inaelekeza maeneo yote ya
kazi nchini kuwa na Mifumo madhubuti ya kuwakinga Wafanyakazi dhidi ya ajali na
magonjwa yatokanayo na kazi.
Aidha, kwa kutambua umuhimu wa Usalama na Afya Mahali pa
Kazi, Wizara yangu ilitunga Kanuni ya 105 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za
Mwaka 2022 inayoelekeza Waajiri kuchukua tahadhari zote dhidi ya ajali na
magonjwa mahali pa kazi.
Nichukue fursa hii kuwapongeza sana OSHA kwa kuendelea
kuisimamia Sheria hii na kuhakikisha kuwa Waajiri wanasimamia kikamilifu
masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi ili kuwakinga watumishi wa Umma dhidi
ya magonjwa, ajali na hata vifo.“ alisema
Waziri Simbachawene alitumia fursa hiyo pia kutoa pongezi kwa
OSHA kwa kuendelea kusimamia vyema utekelezaji wa sheria hizi na kuhakikisha
waajiri wanachukua hatua za kujikinga na kuwalinda wafanyakazi wao.
“Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha wafanyakazi wa umma
wanalindwa na kuwa na mazingira salama ya kazi. Tunapojali usalama wa
wafanyakazi wetu, tunajenga Taifa lenye nguvu kazi imara,” aliongeza.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma,
Mhe. Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola, alielezea kuwa ziara hiyo ni sehemu ya majukumu
ya tume ya kufanya ukaguzi wa utekelezaji wa sheria mbalimbali za utumishi wa
umma
Alisema kuwa Tume imejiwekea utaratibu wa kufanya ukaguzi
katika taasisi mbalimbali na kwamba ziara hiyo inatoa fursa ya kuzungumza na
wafanyakazi kuhusu masuala ya nidhamu na usalama.
“siku ya leo
nimefarijika kushiriki nanyi OSHA katika kikao hiki baada ya kumaliza ukaguzi
vilevile niwajuze kuwa tume hii katika kutekeleza jukumu lake la ukaguzi
imejiwekea utaratibu ambapo viongozi wanapata nafasi ya kutembelea taasisi
ambayo inakaguliwa kama ilivyofanyika leo
Kwa upande wake
Mtendaji Mkuu wa OSHA Bi. Khadija Mwenda alisema taasisi hiyo itaendelea
kusimamia maagizo yote yaliyotolewa, kwa kuendelea kusimamia na kufanya kaguzi
na kutoa elimu ya usalama na Afya na Afya Mahali Pa kazi.
“utekelezaji huu ndani ya serikali ni ishara kuwa Mhe. Rais
Dkt Samia Suluhu Hassan anathamni wafanyakazi wa Tanzania kwa kutambua kuwa
Taifa linahitaji nguvu kazi yenye afya ili kuleta maendeleo tarajiwa.
Lengo la OSHA ni kuhakikisha tunajenga nguvu kazi yenye afya
na usalama kwa kuhakikisha kuwa maeneo ya kazi yanasimika mifumo ya kulinda
wafanyakazi, ambapo kwa sasa tuna imani serikali ikiwa kama mwajiri na mtunga sera mbalimbali ni matarajio yetu kuwa waajiri wote
watazingatia hili ili tulinde nguvu kazi ya taifa” alisema Bi. Khadija Mwenda.
Naye Bwana Mathew Kirama Katibu, Tume ya Utumishi wa Umma
Umma amesema jukumu la Tume ya Utumishi wa Umma ni Kuhakikisha kuwa
sera,sheria,Kanuni,Taratibu na miongozo hiyo inayotolewa na Ofisi ya Rais,Menejmenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inazingatiwa ipasavyo, na Tume hutekeleza
jukumu hilo kupitia ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria katika usimamizi wa
utumishi wa Umma. Ambapo katika ukaguzi huo jumla ya taasisi za Umma zipatazo
160 zimekaguliwa kwenye vipengele 13 kuhusiana na uzingatiaji wa sheria.
.........................................Mwisho................................................
Post a Comment