************
Na Ofisi ya Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri
wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa mwaka 2015, Tanzania iliunga
mkono Ajenda ya Mpango wa Kimataifa wa Usalama wa Afya na kuharakisha
utekelezaji wa Sheria za Afya za Kimataifa ili kuzuia magonjwa ya kuambukiza
kusambaa kimataifa.
Kupitia tathimini ya pamoja
ya mwaka 2023 matokeo ya maendeleo ya Tanzania katika suala hilo inaonyesha
hatua kubwa ambapo mwaka 2016 imedhihirika
azma imara ya Serikali katika kutekeleza Sheria za Afya za Kimataifa kwa
kutumia njia moja ikikubali uunganishaji wa afya ya binadamu, wanyama, na
mazingira.
Dkt. Biteko amesema hayo
leo Novemba 13, 2024 katika ufunguzi wa Kongamano la 14 la Kimataifa la Sayansi
la Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya (CUHAS) lililofanyika jijini
Mwanza lenye kaulimbiu “Afya Moja na Usalama wa Afya wa Kimataifa”.Ametaja
jitihada zilizofanywa na Serikali za kuhuisha miongozo na mipango kazi ili
kutekeleza Ajenda ya Mpango wa Kimataifa wa Usalama wa Afya.
“Mwongozo wa Kitaifa wa Maabara na Usalama wa
Bioteknolojia, Ajenda ya Mpango ya Kazi wa Taifa wa Usalama wa Afya, Mpango wa Mkakati wa Afya
Moja (2022-2027), Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Usugu wa Vimelea vya
Magonjwa dhidi ya Dawa (UVIDA 2023-2028). Pamoja na kuhamasisha ukuzaji na
uendelezaji wa raslimali watu na kuchochea ushirikiano wa kisekta,” amesema
Dkt. Biteko.
Ameendea kusema kuwa Rais
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya jitihada za kuhakikisha
Usalama wa Afya wa Kimataifa hasa kwa kutoa ufadhili wa masomo na mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu kwa lengo la kuongeza nguvu kazi kila mwaka.
“Serikali ya Awamu ya Sita
chini ya uongozi wa Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inathamini mchango
wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi
za Afya pamoja na Kituo cha Tiba cha Bugando kwa ushirikiano na washirika wa ndani
na kimataifa kwa kuwa mabingwa katika nyanja mbalimbali za utafiti
zinazohusiana na Usalama wa Afya wa Kimataifa,” ameeleza Dkt. Biteko.
Ameongeza “Pia Serikali
inathamini mchango uliotolewa na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya
kuanzia mwaka 2007 hadi 2023, ambapo kimezalisha zaidi ya wataalamu wa Afya
7,000 katika fani mbalimbali za tiba, dawa, uuguzi, maabara na uchunguzi wa
kiafya, na uchomaji wa mionzi ambao wamekuwa mabingwa katika Usalama wa Afya ya
Kimataifa.”
Aidha, Dkt. Biteko
ameipongeza CUHAS kwa kuandaa makongamano hayo ya kisayansi yanayojadili
masuala ya kisera ili kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya afya na
kusema kuwa afya ya binadamu inakumbwa na matishio mengi ili kukabiliana nayo
ni lazima kufanya utafiti.
“Nawapongeza kwa kuleta
wataalamu kwa ajili ya kujadili masuala ya tiba, niwapongeze pia kwa ugunduzi
wa aina ya kirusi kinachoitwa Bugandosis ambacho kimebadilisha mfumo wa tiba na
kutoa mchango katika sekta ya afya.
Fauka ya hayo amempongeza
Prof. Stephen Mshana kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya kwa
kuwa mwanasayansi bora kwa mwaka 2024.
Kwa upande wake, Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga amemshukuru Rais
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha sekta ya umma na binafsi hususan
katika elimu na afya, akitolea mfano kupitia mradi wa Elimu ya Juu na
Mabadiliko ya Uchumi (HEET).
Mradi ambao umesaidia elimu
ya juu na kuwezesha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ikiwemo kutoa
ufadhili wa masomo kwa wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za
Afya.
Mhe. Kapanga ameongeza kuwa
Afya Moja inasisitiza kutafuta suhulu ya pamoja ya changamoto ngumu za kiafya
na kuwa Kongamano hilo linasaidia wataalamu, wanasayansi na watunga sera
kujadiliana kwa pamoja Usalama wa Afya.
“Ni matumaini yangu
tutanufaika kutokana na utaalamu na matokea ya tafiti zilizofanyika awali na
mikakati itakayosaidia kupunguza matishio ya afya, nakishukuru Chuo Kikuu cha
Kikatoliki cha Sayansi za Afya kwa kuandaa Kongamano hili,” amesema Mhe.
Kipanga.
Naye, Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya Bugando (CUHAS), Prof. Erasmus
Kamugisha amesema kuwa kauli mbiu ya Kongamano hilo Afya Moja inalenga kuleta
muunganiko wa binadamu, wanyama na afya ya mazingira ambayo inaathiri jamii,
taifa na dunia katika kufikia matokeo bora ya afya.
Ameongeza kuwa Kongamano
hilo linalofanyika kila mwaka limehudhuriwa na takribani washiriki 500 kutoka
nchi mbalimbali duniani na litakuwa na tafiti za sayansi 150 zitakazojadiliwa
kwa siku mbili.
Inaelezwa kuwa tafiti
mbalimbali zinazowasilishwa kupitia makongamano hayo zimeweza kushawishi
kubadilishwa kwa miongozo au sera za huduma za afya nchini ikiwemo mabadiliko
ya dawa.
Aidha, kwa mwaka 2024
yamechapishwa jumla ya machapisho 271 kuhusu mada mbalimbali za tafiti.
=MWISHO=
Post a Comment