UFAFANUZI KUHUSU KIFO CHA MGOMBEA UENYEKITI KWA TIKETI YA CHADEMA , ALIPATA AJALI KABLA HAJAFARIKI,


***************

Jeshi la Polisi Nchini limesema kuwa imeushuhudia kupitia mitandao ya kijamii ikitolewa taarifa ya  kutaka kuupotosha umma kuhusiana na kifo cha Joseph Remigius,Miaka 52 mkazi wa Kijiji cha Karagara,Wilaya ya Misenyi Mkoa wa Kagera ambaye alikuwa ametia nia ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji kupitia Chama cha  Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Akitoa taarifa hiyo Msemaji wa Jeshi la Polisi DCP David Misime amesema kuwa taarifa hiyo sio sahihi ni ambapo ameweka wazi kuwa  Oktoba 31,2024 Joseph Remigius majira ya saa tatu usiku akiwa anatoka kwenye Bar waliyokuwa wanakunywa pombe akiwa amebebwa na bodaboda walipata ajali na baada ya ajali hiyo walipata msaada na kufikishwa katika Kituo cha Afya Minziro na kupatiwa matibabu na kuruhusiwa.

DCP Misime ameongeza kuwa Novemba 1,2024 majira ya saa kumi na dakika ishirini alfajiri ndipo zikapokelewa taarifa katika Kituo Kidogo cha Polisi Minziro kuwa Joseph Remigius amefariki dunia akiwa nyumbani kwake.

Sambamba na hayo amebainisha kuwa hadi sasa kulingana na ushahidi wa mashuhuda wa ajali na waliompatia msaada na kumfikisha katika Kituo cha Afya Minziro, ajali ndiyo chanzo cha kifo chake.

Msemaji wa Jeshi hilo akatoa wito kwa wananchi kuwa endapo kuna mwenye ushahidi tofauti na huo wa mashuhuda wa ajali basi aufikishe Polisi ili ufanyiwe kazi.

0/Post a Comment/Comments