Jeshi la Polisi limewakamata na kuwahoji watuhumiwa wawili kwa kosa la kuharibu kwa kuvunja vioo viwili vya treni ya Mwendo Kasi (SGR) kwa kutumia mawe.
Taarifa iliyotolewa na msemaji wa jeshi la polisi DCP David Misime imeeleza
kuwa Tukio hilo lilitokea Novemba 22, 2024 majira ya mchana katika Kijiji cha
Manase Wilaya ya Chamwino katika Jiji la Dodoma wakati Treni ya Mwendo Kasi
inapita ikitokea Jijini Dar es Salaam kuelekea Jijini Dodoma.
Baada ya tukio hilo kutokea, Jeshi la Polisi lilifanya msako na kufanikiwa
kuwakamata Erasto Michael Richard, Miaka 16 na Hassan Ezekiel Ndahani, Miaka 12
wote wakazi wa Kijiji cha Manase Wilaya ya Chamwino.
Chanzo cha kufanya uharibifu huo ni baada ya kuona treni ikipita wakarusha mawe
kwa pamoja ili kuona kama mawe waliyorusha yataweza kushindana na mwendo wa
treni.
Jeshi la Polisi limetoa wito hasa kwa wananchi wanaoishi maeneo ambayo treni ya
kisasa inapita kuendelea kupeana elimu juu ya umuhimu wa kulinda miundombinu ya
treni hiyo kwani ipo kwa ajili ya manufaa yetu sote.
"kila mzazi/mlezi anaowajibu wa kutoa elimu kwa familia hasa watoto kuacha
vitendo ambavyo vitasababisha uharibifu kwa reli na treni ya kisasa kwani
itawasababisha kukinzana na sheria za nchi." - Amesema DCP David Misime
Post a Comment