ALIYETUHUMIWA KUVAMIA KWA FATUMA NA KUBAKA ATUPWA JELA MIAKA 30


..........................

Na Daniel Limbe,Chato

MKAZI wa kata ya Bwanga wilayani Chato mkoani Geita,Lukas Albogast(33) amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela,baada ya kupatikana na hatia ya kubaka binti mwenye umri wa miaka 14 kinyume cha sheria za nchi.

Katika kesi hiyo namba 8746 ya mwaka 2024 mshitakiwa alikuwa akikabiliwa na makosa mawili tofauti ambapo kosa moja ameachiwa huru na la pili kutiwa hatiani.

Kabla ya kutolewa hukumu hiyo,mwendesha mashitaka kutoka ofisi ya mashitaka,Mauzi Lyawatwa,aliieleza mahakama hiyo kuwa mshitakiwa alitenda makosa hayo Machi 3,2024 kwenye kijiji cha Rwantabe kata ya Bwanga wilayani Chato, majira ya saa za usiku ambapo pasipo ridhaa ya mwenye nyumba mshitakiwa alivamia na kuvunja mlango kwa kutumia jiwe kubwa maarufu(Fatuma).

Amesema baada ya kufanikiwa kuingia ndani,alimweka chini ya ulinzi binti mwenye umri wa miaka 14 (jina limehifadhiwa) aliyekuwa amelala sebuleni kabla ya kuwafungia wazazi ndani ya chumba chao kwa kutumia komeo la mlango.

Akiwa amekusudia kufanya uhalifu huo, mshitakiwa alianza kutoa amri ya kuwataka wazazi wa binti huyo kutoa fedha haraka vinginevyo ataondoka na binti yao na kutokomea kusikojulikana.

Aidha katika hali isiyotarajiwa, mshitakiwa aliondoka na binti huyo baada ya wazazi kudai hawana pesa na alitokomea naye porini na kumlazimisha kufanya naye mapenzi huku akiwa amepora runinga pamoja na simu ndogo aina ya tekno.

Mwendesha mashitaka huyo,amesema kitendo cha kufanya unyang'anyi wa kutumia silaha ni kosa kisheria kwa mujibu wa kifungu namba 387 A sura ya 16 ya kanuni ya adhabu iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Na kwamba kosa la pili(Ubakaji) ni kinyume na kifungu cha 130 (1) (2) (e) pamoja na kifungu 131(1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Hata hivyo,ameiomba mahakama hiyo kumpatia adhabu kali mshitakiwa kutokana na makosa aliyotenda ili liwe fundisho kwa watu wengine,huku akisema ofisi yake haina kumbukumbu ya makosa mengine ya mshitakiwa huyo.

Baada ya mahakama kupitia ushahidi uliowasilishwa mbele yake, ikiwemo jiwe lililotumika kuvunja mlango(Fatuma), fomu maalumu ya matibabu kutoka polisi(PF3) fomu maalumu ya utambuzi wa mtuhumiwa, maelezo ya mashahidi watano akiwamo daktari, maelezo ya ungamo pamoja na onyo yaliyofanywa na mlinzi wa amani,umeisaidia  mahakama hiyo kutoa uamuzi wa haki.

Kabla ya kutolewa hukumu hiyo,na hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo,Erick Kagimbo,mshitakiwa alipewa haki ya kuomba kupunguziwa adhabu ambapo ameomba kusamehewa kwa madai kuwa anategemewa na familia na kwamba ana watoto watatu wanaotegemea mahitaji muhimu kutoka kwake.

Akisoma huku hiyo,Hakimu Kagimbo,amesema kutokana na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka pamoja na utetezi wa mshitakiwa katika kosa la kwanza la unyang'anyi wa kutumia silaha, mahakama hiyo inamwachia huru.

Aidha katika kosa la pili la ubakaji, ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo umetosha kuishawishi mahakama pasipo kuacha shaka kubwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha sheria na kwamba mshitakiwa atakwenda kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Mshitakiwa amepelekwa kwenye gereza la wilaya ya Chato kuanza kutumikia adhabu yake,huku mahakama hiyo ikimpa nafasi ya kukata rufaa iwapo atakuwa hajaridhika na uamuzi wa mahakama hiyo.

                          Mwisho.

0/Post a Comment/Comments