********Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini
(IGP), Camillus Wambura kulisimamia Jeshi la hilo kufanya ukaguzi wa vyombo vya
moto barabarani, kuimarisha doria (highway patrol) usiku na mchana pamoja na
kuimarisha ulinzi kwenye Nyumba za Ibada katika kipindi cha sikukuu za
Christmass na Mwaka Mpya.
Bashungwa ametoa maagizo hayo, leo tarehe 18 Disemba, 2024
wakati akitoa taarifa kwa Umma kuelekea Sikukuu za Mwisho wa Mwaka ambapo
amewahakikishia wananchi na Watanzania wote kuwa nchi iko salama.
“Hatuko tayari kuacha tabia za kizembe ziendelee kupoteza
maisha ya watu, na wengine kupata ulemavu, huku Sheria za kudhibiti uzembe
zikiwa zipo. Tutachukua hatua kali kwa madereva na wasafarishaji wazembe.
Ninaomba wasafiri mtupe ushirikiano, na kuunga mkono jitihada hizi, ili tuwe
salama tunapokuwa barabarani”amesema Bashungwa
Bashungwa ametoa wito kwa wasafiri na wasafirishaji,
kuzingatia na kuheshimu Sheria za Usalama Barabarani, ili kupunguza ajali
zinazoepukika ambazo zimekuwa zikisababisha vifo, majeruhi na hata kusababisha
ulemavu kwa wananchi.
“Nitoe tahadhari kwa familia zinazotumia magari yao binafsi,
kufanya matengenezo ya magari kabla ya safari, na kuacha utamaduni wa kuchukua
mtu yeyote ambaye hana taaluma ya udereva, wala leseni, na hajapitia mafunzo ya
kuendesha magari kwa kukwepa gharama. Kila familia ichukue tahadhari, hususani
tunapoelekea mwisho wa mwaka.”
Aidha, Bashungwa ameliagiza Jeshi la Polisi
kushirikiana na TANROAD pamoja na TARURA
kukagua maeneo yote nchini yenye vizuizi na vituo vya ukaguzi, kuangalia kama
vimewekwa kwa kuzingatia sheria, na tahadhari ya usalama kwa watumiaji wengine
wa barabara na kama vipo katika maeneo hatarishi viondolewe.
“Pale itakapokutwa vizuizi ama vituo vya ukaguzi vimewekwa
bila kuzingatia taaluma na uzingatiaji usalama wa watumiaji wengine wa
barabara, wakutane na Taasisi au Mamlaka husika ili kuviondoa katika maeneo
hatarishi, na kwa pamoja kukubaliana maeneo sahihi ya kuweka vituo hivyo”
amesisitiza Bashungwa.
Kadhalika, Bashungwa amemuagiza IGP Camillus Wambura na
Jeshi la Polisi kwa ujumla kuendelea na operesheni Maalum katika mikoa yote nchini ya kupambana na wezi
na wahujumu wamiundombinu ya TANESCO, SGR, barabara na miundombinu mingine na
watuhumiwa wanaokamatwa, upelelezi ukamilike mapema na kufikishwa kwenye vyombo
vya sheria.
Ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari kubwa katika
maeneo yenye mikondo ya maji inayokatiza barabarani pamoja na wazazi na walezi
kutoacha watoto kuvuka pekee yao kwenye maeneo hatarishi ya maji au kuogelea
kwenye madimbwi kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya
maeneo nchini.
“Upo utamaduni kwenye sherehe za mwisho wa mwaka, wazazi
kuwaacha watoto kwenda sehemu mbalimbali kwa ajili ya kusherehekea sikukuu,
yakiwemo maeneo ya ufukweni au kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya michezo
ya watoto, huku wakiwa peke yao. Niwaombe wazazi kuwalinda watoto na kutoruhusu
watoto kwenda kutembea siku za sikukuu wakiwa peke yao” amesisitiza
Pia, Bashungwa ametoa wito kwa Watanzania kuendelea
kumuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuipa ushirikiano Serikali ili
kuifanya nchi kuendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu, na kuwafanya
wananchi kushiriki katika shughuli za
kiuchumi na kijamii.
Post a Comment