CHUO CHA IFM GEITA KUNUSURU MAZINGIRA NA VIUMBE HAI*

Mwonekano wa mbele wa Chuo cha usimamizi wa fedha(IFM) kampasi ya Geita-Chato
Ofisa mazingira,Neema Benson,akipanda mti kwenye chuo cha usimamizi wa fedha(IFM) kampasi ya Geita-Chato
Katibu tawala(Das) wilaya ya Chato,Thomas Dimme, akipanda mti kwenye Chuo cha usimamizi wa fedha(IFM) kampasi ya Geita-Chato
Mkuu wa chuo cha usimamizi wa fedha(IFM) Kampasi ya Geita-Chato, Dkt. Emmanuel Mtani,akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho
Picha ya pamoja kati ya Katibu tawala(Das) wilaya ya Chato,Thomas Dimme,uongozi wa chuo pamoja na baadhi ya wanafunzi
Ofisa Mazingira,kutoka Ofisi ya mazingira halmashauri ya wilaya ya Chato,akizungumza na vyombo vya habari

.....................

Na Daniel Limbe,Chato

"JAMII yoyote isiyopenda mazingira yake haiwezi kuzaa matunda chanya katika ulimwengu wowote ule" ndivyo wasemavyo wahenga.

Kutokana na ukweli huo, Chuo cha Usimamizi wa fedha (IFM) kampasi ya Geita kilichopo wilayani Chato mkoani humo kimeanza mkakati kabambe wa utunzaji wa mazingira, kupanda miti ya kupasua mbao,matunda pamoja na vivuli ili kulinda uoto wa asili na viumbe wengine hai.

Mkurugenzi wa Chuo cha (IFM),Dkt. Emmanuel Mtani, amesema ili maendeleo ya watu yaweze kupatikana kwa haraka suala la utunzaji mazingira lazima lipewe kipaumbele na liwe endelevu kwa maslahi mapana ya sasa na baadaye.

"Mazingira yetu yanapokuwa salama inatusaidia kama jamii kuishi kwa furaha na amani,ndiyo maana sisi kama Chuo cha usimamizi wa fedha kampasi ya Geita tumekuja na mkakati wa kuhakikisha mazingira yetu yanakuwa ya kuvutia kwa kufanya usafi na kupanda miti mingi ambayo itasaidia kupatikana matunda,hewa safi na vivuli kwaajili ya mapumziko ya wanafunzi wetu"amesema Dkt. Mtani.

Pia ameeleza kuwa utunzaji wa mazingira ni njia ya kuheshimu uumbaji wa mwenyezi Mungu ambaye ndiye mwanzilishi mkuu wa mazingira kabla ya kukabidhi kwa wanadamu kwaajili ya kuendeleza.

Ofisa mazingira kutoka ofisi ya Mazingira halmashauri ya wilaya ya Chato,Neema Benson, amesema mkakati wa wilaya hiyo ni kupanda miti isiyopungua milioni 1.5 kwa kila mwaka na kwamba kupelekea maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika(Tanzania bara) takribani miche 230,000 imepandwa maeneo mbalimbali ikiwemo chuo cha usimamizi wa fedha(IFM) Kampasi ya Geita.

Amesema halmashauri hiyo imejipanga kuhakikisha miche yote iliyopandwa inakua na kustawi vizuri kutokana na elimu inayoendelea kutolewa kwa jamii, taasisi binafsi na serikali ili kuwa na mazingira mazuri na yenye kuvutia na salama kwa afya za binadamu.

"Tunaendelea na mkakati wa kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka,tunaamini baada ya miaka 10 ijayo tutakuwa na Chato ya kijani kila sehemu,ndiyo maana tunasisitiza miche iliyopandwa itunzwe vizuri kunusuru fedha nyingi zilizowekezwa na serikali katika uoteshaji wa miche hiyo"amesema....

Katibu tawala (Das) wilaya ya Chato, Thomas Dimme, amesema Tanzania inapoelekea kuadhimisha miaka 63 ya uhuru disemba 9 mwaka huu,jamii haina budi kujivunia maendeleo makubwa yaliyopatikana tangu utawala wa awamu ya kwanza ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere hadi awamu ya sita inayoongozwa na rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema kabla ya uhuru wa Tanzania bara mwaka 1961 wananchi hawakuwa na usawa wa kupata elimu ukilinganisha na sasa ambapo hata watoto wanaotoka familia duni na maskini wote wanapata elimu sawa na wengine na kwamba hayo ndiyo manufaa ya kujitawala wenyewe.

Amesisitiza jamii kuendelea kushikamana kwa kulinda na kudumisha amani iliyoasisiwa na viongozi na wapigania uhuru wetu kwa madai kuwa amani ndiyo msingi mkuu wa maendeleo yetu kama nchi, na kwamba ipo mikakati mizuri inayoandaliwa na serikali kuhakikisha kila mtanzania anajivunia kuzaliwa katika nchi hii.

"Msisitizo wangu kuelekea maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanzania bara ni wananchi wote tushikamane kuilinda amani yetu kwa kuwa ni tunu muhimu tuliyoachiwa na waasisi na wapigania uhuru wetu, tusikubali kugawanyika kwa sababu ya udini,ukabila,ukanda na tofauti ya rangi zetu"amesema Dimme.

"Ili jamii yoyote iweze kuendelea kiuchumi,kisasa na kiutamaduni utunzaji wa mazingira ni chachu katika kufanikisha ndoto hiyo".

                      Mwisho.

0/Post a Comment/Comments