DC BURA: WANANCHI MUULINDE KWA WIVU MKUBWA MRADI WA MIJI 28

Katikati ni mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura,na kulia ni Mkurugenzi wa mamlaka ya maji Chato mjini,Isack Mgeni.Mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura,akizungumza na wananchi.Sehemu ya mwonekano wa tenki kubwa la maji kwenye kijiji cha Ilyamchele.Utandazaji wa mabomba ya maji ukiendelea.

....................

Na Daniel Limbe,Chato

SERIKALI wilayani Chato mkoani Geita imewataka wananchi wa wilaya hiyo kulinda,kuendeleza na kutunza miundo mbinu ya mradi mkubwa wa maji kutoka ziwa viktoria kwa lengo la kuboresha ustawi wa maisha ya wananchi.

Mradi huo ambao ni miongoni mwa ile inayotekelezwa kwenye miji 28 nchini unatarajiwa kukamilika disemba 2025 kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 38 ikihusisha ujenzi wa chanzo kikuu cha maji,tanki lenye uwezo wa kukusanya lita milioni 3 za maji,kutandaza mabomba pamoja na kutibu maji.

Akiwa eneo la mradi katika ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo kwenye Kijiji cha Ilyamchele,mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura, amesema serikali imetoa fedha nyingi kwaajili yakusaidia huduma ya maji kwa wananchi wa wilaya hiyo na kwamba itakupunguza adha kwa wananchi waliokuwa wakiteseka kwa kukosa huduma hiyo muhimu.

Aidha ametumia fursa hiyo kuwaonya watu wote wenye nia ya kuhujumu miundombinu ya mradi huo na kwamba serikali haitakuwa na huruma na yeyote atakayebainika kudhoofisha jitihada hizo.

"Maji ni uhai na yeyote atakayetaka kuhujumu miundombinu hii hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake pasipo kutazama nafasi yake katika jamii".

"Sitokubali watu wachache watuharibie nia njema hii ya serikali ya mama Samia kwa wananchi wetu,mradi huu ni mkubwa na wenye manufaa mapana kwa umma, tuhakikishe miundombinu hii tunailinda kwa wivu mkubwa ili idumu zaidi ya miaka 100"amesema Bura.

Hata hivyo amempongeza mkurugenzi wa mamlaka ya maji mjini kwa usimamizi mzuri wa mradi huo,huku akimtaka kusimamia vyema pesa za serikali ili zitumike kama zilivyokusudiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari,Mkurugenzi wa mamlaka hiyo,Mhandisi Isack Mgeni,amesema mradi huo unatarajiwa kuwanufaisha wananchi zaidi ya 100000 na kwamba utasaidia kupunguza mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza ikiwemo,kichocho,kipindupindu na hata minyoo.

Amesema mamlaka hiyo inakusudia kukamilisha mradi huo disemba 2025 ambapo kukamilika kwake itasaidia wananchi kupata maji safi na salama hadi majumbani mwao ukilinganisha na hali ilivyo sasa ambapo mjini Chato wanapata maji kwa aslimia 60 pekee.

Hata hivyo,amesema mradi huo ambao umefikia aslimia 26 ya ujenzi wake, utakuwa na uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 10 ambazo zitasambazwa maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Mbali na kuipongeza serikali kwa ujenzi wa mradi huo,diwani wa kata ya Ilyamchele, Phares Luhangija, amesema moja ya manufaa ya mradi huo ni kusaidia uzalishaji wa chakula kutokanana na kuimalishwa kilimo cha umwagiliaji na bustani za mboga mboga.

Kadhalika itasaidia kuongezeka kwa mapato ya halmashauri kutokana na tozo zitakazokusanywa kupitia mazao yatakayozalishwa.

"Binafsi naona serikali ikienda kutatua changamoto ya muda mrefu kwa wananchi,

sambamba na falsafa ya kumtua mama ndoo kichwani,tutarajie mafanikio makubwa sana maana muda wa kuhangaika kutafuta maji sasa utatumika kwenye kazi za kuzalisha mali ili kuinua uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla" amesema Luhangija.

                      Mwisho.





 

0/Post a Comment/Comments