KAMISHNA MKUU WA TRA AAHIDI USHIRIKIANO KWA WALIPAKODI ARUSHA

********

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Mwenda ameahidi kuendelea kushirikiana na Walipakodi mkoani Arusha na kueleza kuwa katika mwezi Disemba ambao ni mwezi wa Shukurani kwa walipakodi hatakaa ofisini, badala yake atawafuata walipakodi kwenye maeneo yao na kuwasikiliza huku akiwapa Shukurani.

Akizungumza na mmoja wa wafanyabiasha wanaounda magari ya kubebea Watalii jijini Arusha Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wafanyabiasha pamoja na wawekezaji katika maendeleo ya Taifa kupitia kodi wanazolipa.

Amesema kwa kutambua thamani ya walipakodi ameamua kuwafuata na kuwashukuru ili kuwapa motisha ya kuendelea kulipa kodi hali ambayo itaboresha mazingira ya walipa kodi hao wakitambua kuwa wao na TRA siyo maadui na wanajenga nyumba moja.

"Mameneja wote nimewapa maelekezo kuwa hakuna kukaa ofisini, watoke wakawasikilize walipakodi na kuona mazingira yao ya ufanyaji kazi pia kutoa Shukurani huku wakitatua changamoto walizonazo, hii itasaidia sana kuwajengea walipakodi imani" Kamishna Mkuu Mwenda.

Akiwa katika Ofisi za World Vision Tanzania mkoani Arusha Kamishna Mkuu Mwenda amesema Shirika hilo lililoajiri wafanyakazi takribani 500 wamekuwa ni walipakodi wazuri wasiokuwa na udanganyifu katika kodi na wanaozingatia sheria. 

Bw. Mwenda amesema yapo mashirika mengi yanayofanya kazi za kijamii yanayofanana na World Vision lakini yamekuwa siyo walipaji wazuri wa kodi na kuwataka kuiga mfano wa World Vision kwa uaminifu katika kulipa kodi.

"World Vision inafanya kazi katika mikoa 15, angalieni uwezekano wa kwenda mikoa mingine mpaka Visiwani Zanzibar,  maana mmekuwa na msaada mkubwa kwa jamii yetu hasa kwa watoto waliopo katika mazingira hatarishi na jamii zisizokuwa na uwezo" Kamishna Mkuu Mwenda. 

Amewaambia World Vision kwamba milango ipo wazi kwa World Vision kufanya mazungumzo na TRA kuhusu masuala ya kikodi waliyoomba kusaidiwa na mazungumzo hayo yatafanywa kwa kufuata sheria ili kuweka usawa kwa kila upande. 

Kamishna Mkuu Mwenda pia ametembelea Kampuni ya Enza Zaden Africa inayomiliki shamba za kuzalisha mbegu na kujionea uendeshaji wa shughuli zao huku akiwapongeza kwa kukua na kuwa walipakodi wa kati na waaminifu katika ulipaji kodi.

Kwa upande wao baadhi ya walipakodi waliotembelewa akiwemo Satbir Singh Hanspaul ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Hanspaul inayounda magari ya kubebea watalii amesema ni mara ya kwanza kutembelewa na kiongozi wa ngazi ya juu wa TRA jambo ambalo litawapa morali zaidi ya kulipa kodi na kuchangia pato la Taifa.

Mkurugenzi huyo amesema katika kipindi cha karibuni kumekuwa na mazingira rafiki ya ukusanyaji kodi yanayotoa ahueni kwa mlipakodi kutokana na kuwepo kwa utaratibu wa kusikilizwa pale panapotokea changamoto katika mazingira yao ya kazi.

Naye Mkurugenzi wa Miradi World Vision Tanzania Bi. Nesserian Mollel amesema shughuli wanazofanya zinaisaidia jamii ya Tanzania mijiji na bijijini na wamekuwa wakilipa kodi kwa uaminifu hata kwa mizigo wanayoingiza nchini kutoka kwa wahisani nje ya nchi kwaajili ya kuwasaidia watanzania. 

Amesema kutembelewa na Kamishna Mkuu wa TRA kumewapa motisha ya kuendeleza uaminifu katika kulipa kodi na kuwa wataitumia vizuri fursa ya mazungumzo na TRA ili wapate ahueni ya kodi.

Mwakilishi wa Kampuni ya kuzalisha mbegu ya Enza Zaden Africa Gerald Matowo ambaye ni Meneja uendeshaji amesema wanajivunia kuwa walipakodi wazuri waliotambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA na kuwa wataendeleza uaminifu huo.

Kamishna Mkuu wa TRA yupo ziarani katika mikoa mbalimbali nchini kutoa Shukurani kwa Walipakodi na kuwasikiliza.













Mwisho




0/Post a Comment/Comments