Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema
Kongamano la Wafanyabiashara na
Wawekezaji nchini Saudi Arabia litaongeza uwekezaji kwenye Sekta ya
Nishati kutokana na Tanzania kuzinadi fursa zilizopo kwenye maeneo mbalibali
ikiwemo Gesi Asilia, Umeme na Nishati Safi ya Kupikia.
Mhe. Kapinga amesema hayo katika Kongamano la
Wafanyabiashara na Wawekezaji zaidi ya 250 kutoka Tanzania na Saudi Arabia
linalofanyika tarehe 18 na 19, Disemba, 2024 katika Mji wa Riyadh nchini Saudi Arabia.
Amesema kuwa, Kongamano hilo ni muhimu kwa upande wa Wizara
ya Nishati na nchi kwa ujumla kwa kuwa linatangaza fursa zilizopo nchini katika
uwekezaji kupitia Sekta ya Nishati ikizingatiwa kuwa kwa sasa Tanzania inavyanzo vingi vya
kuzalisha umeme mwingi na wa uhakika likiwemo Bwawa la Julius Nyerere ambalo
litazalisha jumla ya Megawati 2,115.
" Kongamano hili litaendelea pia kujenga mahusiano
mazuri kati ya Tanzania na Wadau kutoka Saudi Arabia katika Sekta ya
Nishati." Amesema Kapinga
Akifungua Kongamano hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, aliwakaribisha wawekezaji kuwekeza nchini na kueleza kuwa
Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji
katika Sekta mbalimbali kupitia Sera nzuri, Misingi imara na Rafiki kwa
wawekezaji iliyowekwa.
Aliwakaribisha wawekezaji hao kuwekeza katika nyanja mbalimbali ikiwemo
Nishati, Madini, Viwanda, Biashara, Kilimo, Miundombinu pamoja na
Uchumi wa Buluu.
Profesa Mkumbo alieleza kuwa Sekta ya Uwekezaji nchini kwa
sasa inakua kwa kasi kubwa, ambayo imechagizwa na Sera nzuri zilizopo chini ya
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuhakikisha kuwa wawekezaji wengi
wanakuja kuwekeza nchini ili kukuza uchumi na
kuitangaza Tanzania kote ulimwenguni.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia,
Dkt. Mah’d Juma Abdalla amewaasa watanzania wanaoshiriki kongamano hilo kutumia
vyema fursa hiyo kuitangaza vyema nchi yao na kutanua wigo wa biashara zao kwa
kuwa nafasi hizo ni aghalabu kupatikana.
Amesema kila mshiriki ahakikishe anatimiza lengo
lililompeleka katika nchi hiyo ili aweze kupata matokeo chanya katika sekta
yake baada ya kongamano hilo kumalizika.
Mawaziri mbalimbali
wanaohudhuria Kongamano hilo ni Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt.
Selemani Jaffo, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Madini, Antony
Mavunde na Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Ajira na
Uwekezaji Zanzibar, Sharif Ali Sharif.
Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zake wanaoshiriki Kongamano hilo ni Kamishna
Msaidizi wa Petroli, Mhandisi Joyce Kisamo, Mkurugenzi Msaidizi wa Sera,
Utafiti na Ubunifu, Oscar Kashaigiri na Meneja wa Biashara ya Mafuta wa kutoka
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Baraka Nyakutonya.
Mwisho.
Post a Comment