LISSU ATANGAZA KUGOMBEA UENYEKITI CHADEMA


.......................

Mwanasiasa mashuhuri nchini Tanzania,na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Democrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu,ametangaza kwa msisitizo nia yake ya kuwania nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho na kudai atakuwa tayari kurudi kwenye maridhiano ya kweli. 

Lissu amesema hayo jijini Dar es salaam katika mkutano wake na  waandishi wa habari ambapo ameweka dhamira yake ya kurejesha umoja, mshikamano, na maridhiano ya kweli ndani ya chama na vyama vingine vya siasa nchini.

Lissu amesema kuwa lengo kuu la uongozi wake litakuwa ni kuhakikisha kuwa CHADEMA inakuwa mfano wa kuigwa katika kukuza demokrasia na uwazi akieleza ni muhimu kwa chama kujenga siasa za maelewano zitakazowezesha kufanikisha malengo ya mabadiliko ya kweli kwa Watanzania.

Katika hotuba yake, Lissu amesisitiza umuhimu wa viongozi wa kisiasa kuweka mbele masilahi ya watanzania kuliko masilahi ya kibinafsi huku akiahidi kuwa atafanya kazi kwa kushirikiana na wanachama wote wa CHADEMA ili kuimarisha chama na kuhakikisha kuwa kinaendelea kuwa sauti ya wanyonge nchini.

Mkutano huu wa Tundu Lissu unakuja wakati ambapo CHADEMA inajiandaa kwa uchaguzi wa ndani wa chama na huku mazingira ya kisiasa nchini yakiwa kwenye kipindi cha mabadiliko makubwa. 

Viongozi wengine waliowahi kushika nafasi ya Uenyekiti Taifa wa CHADEMA ni Edwin Mtei, mwanzilishi wa chama hicho, na baadaye 2002 hadi 2003 Bob Makani, ambaye alishika nafasi hiyo baada ya Mtei na Mbowe, anayeshikilia nafasi hiyo kuanzia 2004 mpaka sasa.

0/Post a Comment/Comments