Ujenzi wa
maabara tatu za Sayansi katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kakonko, Kigoma,
umeleta hamasa kubwa ya kitaaluma kutokana na kuboresha mazingira ya kujifunza
na kufundishia.
Maabara hizo
za Fizikia, Kemia, na Biolojia, zilizogharimu shilingi milioni 180, zilijengwa kwa ufadhili wa
Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) kwa kushirikiana na Mfuko wa Elimu wa Taifa
(TEA). Shule hii yenye wanafunzi 270 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne
imepata mwamko mpya wa elimu, jambo lililowaletea furaha walimu na wanafunzi.
Mkuu wa
shule hiyo, Antoria Paul Nkabo, alisema kukamilika kwa mradi huu kutaongeza
hamasa ya wanafunzi kufanya vizuri zaidi katika masomo ya sayansi kutokana na
mazingira bora na rafiki ya kujifunzia kwa vitendo.
“Kwa kupata
mradi huu, tunakwenda kuongeza ufaulu. Tunatarajia nusu ya wanafunzi(167)
watakaoingia kidato cha nne wapate daraja la kwanza katika mitihani yao ya
mwisho,” alisema.
Mwalimu wa
Kemia na Biolojia, Nikolous Kayombo, aliongeza kuwa awali walifundisha masomo
hayo kwa nadharia pekee, lakini sasa, kupitia maabara hizi, wanafunzi wataweza
kujifunza kwa vitendo, hivyo kuongeza uelewa na ufaulu wao.
Wanafunzi
Zulfa Twaha (Kidato cha Kwanza), Happines Amosi (Kidato cha Tatu), na Sharifat
Hamad walitoa shukrani zao kwa UNICEF na TEA kwa kuwapatia maabara hizi muhimu.
Walibainisha kuwa maabara hizi zinawawezesha kufanya majaribio mengi ya masomo
ya sayansi, jambo linalochochea mafanikio yao kitaaluma.
Mbali na
maabara, TEA pia ilitoa ufadhili wa ujenzi wa bweni lenye uwezo wa kuchukua
wanafunzi 120 mwaka 2022/2023, kwa gharama ya zaidi ya TZS milioni 142.9.
Mwanafunzi Sharifat
alieleza kuwa bweni hilo limeboresha makazi yao, hivyo kuwawezesha kujikita
zaidi katika masomo yao.
Shule ya Wasichana Kakonko iliyoanzishwa mwaka 2022 ina jumla ya wanafunzi 274, na mwaka 2025 inatarajia kudahili wanafunzi wengine 100 wa kidato cha kwanza, jambo linaloashiria maendeleo endelevu shuleni hapo.
Post a Comment