Na Daniel Limbe,Chato
WANANCHI wilayani Chato mkoani Geita wamejitokeza kwa wingi kufanya usafi wa mazingira, kupanda miti 230,000 pamoja na kutoa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa waliolazwa kwenye hospitali ya wilaya hiyo.
Uamuzi huo umelenga kuungana na watanzania wengine wakati nchi ikielekea maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika (Tanzania bara) disemba 9,2024 huku serikali ikieleza mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa serikali ya awamu ya kwanza hadi ya sita.
Akizungumza na baadhi ya wananchi wa wilaya ya Chato,mgeni rasmi katika hafra hiyo ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo,Christian Manunga,amesema watanzania hawana budi kujivunia maendeleo makubwa yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka 63 ya uhuru.
Amesema wilaya ya Chato ni miongoni mwa wanufaika makubwa wa miradi ya maendeleo ikiwemo sekta ya elimu,afya,maji,viwanda,vyuo vikuu,vyuo vya kati, ufundi stadi,uwanja wa ndege pamoja na miundo mbinu ya barabara.
"Tunapoelekea kuadhimisha miaka 63 ya uhuru wa Tanzania bara hatuna budi kuyaenzi mema yote yaliyofanywa na waasisi wetu kutoka serikali ya awamu ya kwanza hadi ya sita,kazi kubwa imefanyika na kila mmoja wetu anaona kwa macho yake" amesema Manunga.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Mandia Kihiyo, amesema halmashauri ya wilaya ya Chato inaendelea kutekeleza miradi mingi ya maendeleo kwa lengo la kuinua ustawi wa wananchi na kuboresha maisha ya kila mtanzania kutokana na mipango madhubuti ya serikali.
Kadhalika amesema mafanikio yaliyopatikana miaka 63 ya uhuru yametokana na serikali kushirikiana na jamii katika kupanga na kutekeleza mipango endelevu jambo lililosaidia halamashauri hiyo kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.
Kwa upande wake,Katibu tawala wa wilaya hiyo,Thomas Dimme, amesisitiza utunzaji wa mazingira kwa jamii ikiwa ni pamoja na kupanda miti kila kaya,kufanya usafi,kunawa mikono pamoja na kutumia vyoo bora ili kulinda afya ya jamii.
Pia amezitaka taasisi binafsi na za umma kupanda na kutunza miti kwa manufaa ya sasa na baadaye na kwamba ni aibu kwa nchi kama Tanzania kugeuka jangwa licha ya kuwa na ardhi bora na yenye rutuba nzuri kwa mimea na mazao.
Mbali na mafanikio ya uhuru wa Tanganyika, Katibu wa chama cha Mapinduzi(CCM) wilaya ya Chato,Charles Mazuri,amesema kama siyo vita ya Uganda na Kagera,huenda Tanzania ingekuwa na uchumi kama nchi ya China.
"Kama siyo vita ya Uganda na Kagera mwaka 1978/79 naamini sasa hivi tungekuwa mbali sana kiuchumi kama walivyo wenzetu China,maana baada ya vita ile nchi yetu ilifilisika kiasi kwamba baadhi yetu tulilazimika kufua nguo kwa kutumia magome ya miti".amesema Mazuri.
Kwa upande wake,mwakilishi wa meneja wa TFS wilaya ya Chato,Peter Mwadima,amesema Wakala wa misitu nchini inaendelea kusisitiza jamii kutunza mazingira kwa kutoharibu misitu ya hifadhi kutokana na shughuli za kibinadamu badala yake kila mwananchi aone thamani ya kupanda na kutunza miti kwa matumizi ya baadaye.
Kadhalika amedai TFS wilayani humo imeotesha miche zaidi ya 200,000 ambayo ipo tayari kwaajili ya kupandwa maeneo mbalimbali ya jamii huku wananchi na taasisi zikialikwa kuchangamkia fursa hiyo.
Kuelekea maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanzania bara,kauli mbiu yaaadhimisho hayo inasema "Uongozi madhubuti na ushirikishwaji wa wananchi ni msingi waaendeleo yetu".
Mwisho.
Post a Comment