***
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM mkoani Rukwa Bi. Silafu Jumbe Maufi amewataka wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa kujiepusha na uhujumu wa miundombinu ya Miradi ya TACTIC Mkoani Rukwa, na badala yake wawe walinzi wa miundombinu hiyo katika kuhakikisha kuwa miradi hiyo inatumika kwa muda mrefu na kwa tija.
Bi.Silafu ametoa kauli hiyo mapema leo Ijumaa Disemba 06, 2024 Mjini Sumbawanga kwenye Ukumbi wa Nazareti wakati wa Hafla ya utiaji saini Mkataba wa ujenzi wa Soko kuu la Mazao Eneo la Kanondo Wilayani Sumbawanga Kupitia Mradi wa Uboreshaji Miji Tanzania (TACTIC) Katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Akiishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bi. Silafu amesema mradi huo wa soko utasaidia wakulima wa Rukwa kuongeza thamani kwenye mazao yao ya kilimo na kuondokana na uuzaji wa malighafi uliokuwa unawatia hasara wakulima wengi wa mkoa huo.
Aidha Kiongozi huyo wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Rukwa ameitaja miradi hiyo ya TACTIC kuwa itasaidia katika kupunguza tatizo la ajira mkoani humo kwani Vijana na wanawake wengi watapata ajira kwenye miradi hiyo kwa kuwa na maeneo ya kufanyia biashara na ujasiriamali kupitia vibanda na vizimba vinavyojengwa kwenye miradi ya TACTIC.
Pamoja na ujenzi wa miundombinu, miradi ya TACTIC ina kipengele cha kuzijengea uwezo taasisi zote za Wizara, TARURA pamoja na Halmashauri za Miji kupitia mafunzo mbalimbali yanayolenga kuboresha utendaji kazi, ufanisi wa huduma mbalimbali za kijamii pamoja na kununua vitendea kazi katika kukuza na kuhuisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato.
Post a Comment