NAIBU KATIBU MKUU MABULA AZINDUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO WAHIFADHI WA UTALII TFS


.....................

Katika juhudi za kuimarisha sekta ya utalii nchini, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Ndugu Nkoba E. Mabula, leo Desemba 2, 2024 ameufungua rasmi mafunzo ya kuwajengea uwezo wahifadhi wa utalii katika Hifadhi za Misitu na Vituo vya Malikale nchini, yaliyofanyika jijini Arusha.

Mafunzo haya, yaliyoandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha sekta ya utalii na kuongeza tija katika usimamizi wa maeneo ya utalii wa misitu.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Ndugu Mabula alieleza kuwa sekta ya utalii ni muhimu katika kukuza uchumi wa Taifa, kwa kutoa ajira na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi.

Aliongeza kuwa, sekta hiyo imeendelea kuwa miongoni mwa vyanzo vikubwa vya mapato ya kigeni, ikiwa na mchango wa takriban asilimia 17.2 kwenye Pato la Taifa mwaka 2023, na kwamba idadi ya watalii imeongezeka kutoka 1,527,230 mwaka 2019 hadi 1,808,205 mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 18.

Ndugu Mabula alisisitiza umuhimu wa kuendeleza vivutio vya utalii nchini, akisema kuwa Tanzania ina maeneo ya kipekee kama vile Mbuga za Wanyama, Mlima Kilimanjaro, na Bonde la Ngorongoro, lakini ni muhimu pia kuhakikisha kuwa huduma bora na huduma za kipekee zinatolewa kwa watalii.

"Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inajitahidi kuimarisha sekta hii, ikiwa na malengo ya kupokea watalii milioni 5 na mapato ya dola bilioni 6 ifikapo mwaka 2025," alisema.

Akiendelea, Ndugu Mabula alieleza kuwa pamoja na kuwa na vivutio vya asili vya utalii, Tanzania inapaswa kuongeza juhudi katika kuendeleza utalii wa misitu, ambao bado ni changa katika nchi.

Alisema kuwa sekta ya utalii wa misitu ilianza kupewa msukumo mwishoni mwa miaka ya 2010 na sasa imetengewa nafasi katika Mpango Mkakati wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) 2021-2026.

"Pamoja na kuchelewa, bado tuna nafasi kubwa ya kuonyesha mabadiliko na matokeo makubwa," alisema.

Alitoa wito kwa wahifadhi kuwa wabunifu katika kujitangaza na kutumia teknolojia ya kisasa katika kueneza taarifa kuhusu vivutio vya utalii na kuhakikisha kuwa fursa zilizopo zinatangazwa zaidi.

 "Maisha yako kiganjani mwako, hivyo ni muhimu kutumia njia za kisasa ili kuyafikia makundi mengi na haraka," alisisitiza.

Ndugu Mabula pia alikushukuru wakufunzi kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kuandaa mafunzo hayo na aliwahimiza washiriki kutumia fursa hiyo ya kujifunza kuboresha ufanisi wao katika kazi.

"Mafunzo haya ni sehemu ya mikakati ya kukuza utalii, hivyo ni muhimu mzingatie yale mtakayojifunza na kuhamasisha ubunifu katika maeneo mnayosimamia," alisema.

Wakati huo huo, Ndugu Mabula alithibitisha kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itakuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za TFS katika kukuza utalii wa misitu na malikale, akitolea mfano mradi wa Walkboard uliofanyika Tanga na kutolewa kwa fedha shilingi milioni 200 ili kukamilisha kazi hiyo.

Mafunzo haya, ambayo yatadumu kwa muda wa siku kadhaa, yatashirikisha wahifadhi na maafisa kutoka maeneo mbalimbali ya utalii na hifadhi za misitu, na yatakuwa na lengo la kuimarisha ufanisi katika usimamizi wa utalii wa misitu na kuongeza mvuto wa vivutio vya utalii nchini.

Kwa upande wake Prof. Dos Santos Silayo, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS anasema serikali, kwa msaada wa wadau mbalimbali, inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha sekta ya utalii inakua, huku TFS ikichukua hatua za kuboresha miundombinu, kujiimarisha kidigitali, na kuanzisha miradi ya utalii wa michezo na matukio.

Mwishowe, aliwataka wahifadhi na wadau wote kuendelea kushirikiana ili kuendeleza na kudumisha fursa hizi za kipekee katika misitu ya Tanzania.

Dr. Thereza Mugobi, Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kujenga uwezo kwa wahifadhi wa TFS wanaosimamia utalii, akisisitiza umuhimu wa utalii wa misitu na malikale katika kuchangia maendeleo ya sekta ya utalii nchini. 

Alipongeza juhudi za wahifadhi katika kuibua mazao mapya ya utalii, akisema kwamba ubunifu wao umesaidia kuongeza idadi ya watalii na mapato kutokanayo na utalii.

0/Post a Comment/Comments