Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea kutekeleza Mradi
wa usambazaji wa mitungi ya gesi ya kilo 6 kwa bei ya ruzuku, ambapo inatarajia
kugawa mitungi 13,020 katika mkoa wa Shinyanga, Mradi huo utagharimu jumla ya
shilingi milioni 545.538
REA, iliingia mkataba na mtoa huduma; kampuni ya Lake Gesi,
kampuni ambayo, itahudumia wilaya 4 za Mkoa wa Shinyanga kwa kuuza mitungi hiyo
ya gesi ya kilo 6 kwa bei ya ruzuku ya shilingi 20,950 pamoja na vifaa vyake,
katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji.
Hayo yameelezwa na Mhandisi Miradi wa Wakala wa Nishati
Vijijini-REA Mhandisi Ramadhani Mganga leo tarehe 19 Disemba 2024 wakati
akizungumza na Wakunga, Wauguzi, kina mama waliojifungua watoto njiti na Mama
wajawazito katika Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama na
kuwagawia mitungi ya gesi ya Kilo sita kila mmoja ambapo jumla ya mitungi 100
imetolewa yenye thamani ya shilingi Milioni 4.1
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa REA Bi Martha
Chassama amesema kuwa kazi ya Serikali ni kuhakikisha nishati safi za kupikia
zinawafikia Wananchi wa vijijini kwa ukaribu zaidi na kwa bei nafuu na kuongeza
kuwa Serikali inafanya kwa kushirikiana na Sekta Binafsi.
Chassama amesisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya gesi hizo
walizopewa huku akieleza kuwa wilaya zitakazofikiwa na mradi huo katika mkoa wa
Shinyanga ni pamoja na Kishapu, Shinyanga na Halmashauri ya Ushetu na Msalala.
Mbunge wa Vitimaalum Mkoa wa Shinyanga Mhe Santiel Kirumba
ameupokea mradi huo ambapo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele na kuipa REA fedha kwa
ajili ya kuhakikisha wanawake wanatumia nishati safi na salama ambayo pia
itaokoa muda na afya za watumiaji ikiwemo kuokoa mazingira.
"Nishati salama ni mtaji wa afya zetu, ni mkombozi wa
uchumi, Inaepusha wanawake na ukatili wa kijinsia, hivyo nampongeza sana Mhe
Rais Dkt Samia kupitia taasisi ya REA kwa kumjali mwanamke na watanzania kwa
ujumla wake" Amekaririwa Mhe Kirumba
Post a Comment