*****
Na Daniel Limbe, Chato
KATIKA kuadhimisha miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika(Tanzania bara) Chama cha kuweka na kukopa cha walimu Chato(Chato Teachers Saccos) kimetoa misaada mbambali kwa wagonjwa waliolazwa kwenye hospitali ya wilaya hiyo ikiwa ni kutekeleza maelekezo ya rais Samia Suluhu Hassan,kuadhimisha siku hiyo kwa kufanya mambo ya kijamii.
Baadhi ya misaada hiyo ni pamoja na sabuni za unga kwaajili ya kufulia, mafuta ya kupaka pamoja na sabuni za kuogea ambazo zinathamani ya zaidi ya shilingi 500,000.
Akizungumza na baadhi ya wagonjwa na baadhi ya walimu wa Saccos hiyo, Diwani wa kata ya Chato,Mange Ludomya, amepongeza jitihada za Saccos hiyo kuguswa na mahitaji ya wagonjwa na kuamua kutenga fedha kwaajili ya kusaidia mahitaji mbalimbali.
Amesema kitendo hicho kimekwenda sambamba na maagizo ya rais Samia Suluhu,kuadhimisha miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika kwa kufanya matendo ya kijamii ikiwemo kufanya usafi katika maeneo mbalimbali,kuhudumia wasiojiweza na kupanda miti.
Mwenyekiti wa "Chato Teachers Saccos" Peter Rwegasira,amesema msaada huo umetokana na taasisi hiyo kutenga kiasi cha fedha kutoka faida yake ya mwaka 2024 na kwamba hatua hiyo ni kutii agizo la rais kuhakikisha kila taasisi inaadhimisha siku ya uhuru kwa kufanya matendo ya kijamii.
Amesema uamuzi huo umefanyika muda mchache kabla ya chama hicho kufanya mkutano mkuu wa mwaka 2024 kutokana na muongozo wa sheria,taratibu na kanuni za ushirika.
Mwalimu Bashir Mushumba(mjumbe wa bodi Chato Teachers Saccos),amesema msaada huo umetolewa baada ya bodi ya chama hicho kuamua kuunga mkono maelekezo ya serikali na kwamba ipo haja kwa taasisi zingine kuwahudumia wahitaji japo kwa kidogo ili kuvuna baraka za mwenyezi Mungu.
Mbali na pongezi zilizotolewa na uongozi wa hospitali ya wilaya kwa misaada kwa wagonjwa, Katibu wa hospitali hiyo, Anna Mwangalika,ameitaka jamii kuguswa na mahitaji ya wagonjwa kutokana na baadhi yao kupokelewa eneo hilo wakiwa hawana ndugu wala fedha za kuwasaidia mahitaji mbalimbali.
"Kwa niaba ya uongozi wa hospitali yetu ninatoa shukurani nyingi sana kwa Saccos ya walimu kwa msaada mkubwa waliotoa maana wagonjwa wote wamepata na tumebaki na vifaa vingine ambavyo tutawagawia wahitaji wengine tutakao wapokea hospitalini kwetu".amesema Anna.
Katibu wa hospitali ya wilaya ya Chato, Anna Mwangalika,akizungumza na vyombo vya habari
Baadhi ya wanachama wa Chato Teachers Saccos Chato,wakitembelea wagonjwa
Kulia ni Diwani wa kata ya Chato,Mange Ludomya na kushoto ni mwenyekiti wa Chato Teachers Saccos,Peter Rwegasira,wakisalimia wagonjwa
Mwisho.
Post a Comment