SERIKALI,HOSPITALI YA RUFAA KANDA YA CHATO WATOA MISAADA KWA WAHITAJI

Katibu tawala wilaya ya Chato,Thomas Dimme,akikabidhi juisi kwa watoto wenye mahitaji maalumu waliopo kwenye shule ya msingi Chato
*****

Na Daniel Limbe,Chato

SERIKALI wilayani Chato Mkoani Geita kwa kushirikiana na Hospitali ya rufaa kanda Chato,wametembelea wagonjwa waliolazwa kwenye wodi mbalimbali na kuwapatia misaada ya fedha na mahitaji mengine ya kibinadamu.

Mbali na hospitali hiyo, takribani wanafunzi 91 wenye mahitaji maalumu kwenye shule ya msingi Chato wamefikiwa na kupewa misaada ya chakula vinywaji na fedha taslimu kwa lengo la kuwatia moyo na kuihamasisha jamii kuwajali wahitaji.

Misaada hiyo imetolewa ikiwa ni kuungana na watanzania wengine kuelekea maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanzania bara disemba 9, 2024.

Katibu tawala wa wilaya ya Chato,Thomas Dimme, mbali na kuvutiwa na huduma bora zinazotolewa na hospitali ya rufaa kanda Chato amesema serikali inaendelea kuboresha miundo mbinu ya afya kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora kwa manufaa ya sasa na baadaye.

"Serikali yetu inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ndani na nje ya wilaya yetu,na haya ndiyo matunda kamili ya uhuru tulioupata kutoka kwa wakoloni mwaka 1961"amesema Dimme.

Sambamba na maadhimisho hayo,serikali imewataka wananchi kuyaenzi mema yote yaliyofanywa na waasisi wa taifa letu pamoja na wapigania uhuru wetu kwa kazi kubwa waliyoifanya baada ya ukoloni.

Akizungumza na waandishi wa habari,Mkuu wa kitengo cha magonjwa ya kuambukiza kutoka hospitali ya rufaa kanda Chato,Dkt. Lameck Mabirika,amesema hospitali hiyo imesaidia kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi wengi wa kanda ya ziwa waliokuwa wakilazimika kwenda Hospitali ya taifa muhimbili.

Amesema miaka 63 ya uhuru wa Tanzania bara ni yenye mafanikio makubwa kwenye sekta ya afya ukilinganisha na enzi za ukoloni ambapo huduma za afya zilikuwa duni na zilipatikana kwenye miji mikubwa pekee.

Kwa upande wake, Katibu wa hospitali ya rufaa kanda ya Chato, Fadhila Mwambene,amesema hospitali hiyo imetoa matendo ya huruma kwa wagonjwa ili kuendelea kuwatia moyo na kutambua thamani ya miaka 63 ya uhuru wa Tanzania bara.

"Tumelazimika kutoa misaada kwa wagonjwa wetu waliolazwa kwenye hospitali ya rufaa kanda ya Chato kwa kushirikiana na Ofisi ya mkuu wa wilaya yetu ili kuwafariji na kuwatia moyo kuelekea maadhimisho ya uhuru wa Tanganyika disemba 9 mwaka huu.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Chato,David Msyangi,mbali na kupongeza misaada iliyotolewa na serikali kwa watoto wenye mahitaji maalumu kwenye shule hiyo,ameiomba serikali kuongeza walimu wa elimu maalumu ili kuendelea kuinua taaluma ya kundi hilo ambalo zamani halikupewa kipaumbele katika elimu.

Amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,454 ambapo kati yake wanafunzi 91 ni wenye mahitaji maalumu ambapo 51 kati yake wana ulemavu wa utindio wa ubongo.

Kuelekea maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika kauli mbiu yake inasema "Uongozi madhubuti na ushirikishwaji wa wananchi ni msingi wa maendeleo yetu".



Baadhi ya walimu na wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika picha ya pamoja na katibu tawala wilaya ya Chato(Das),Thomas Dimme.

Katibu tawala wilaya ya Chato,Thomas Dimme, akizungumza na baadhi ya wagonjwa kwenye hospitali ya rufaa kanda ya Chato

                     Mwisho.

0/Post a Comment/Comments