******
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Bw. Hans Christian Stausboll, Mkurugenzi wa Masuala ya Afrika kutoka Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya, yalıyı Po Ubelgiji, kujadili masuala ya ushirikiano katika uchumi wa kidijitali nchini.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo tarehe 11 Desemba, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Waziri Silaa ameeleza kuwa mazungumzo hayo yalijikita zaidi katika ushirikiano baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya hususan katika sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari (TEHAMA), pamoja na kubadilishana uzoefu katika mageuzi ya kidijitali.
Aidha, Waziri Silaa amesema kuwa Tanzania imenufaika na ufadhili kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kupitia mradi wa Digital4 Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano (2021-2025) wenye thamani ya Euro Milioni 35.
Mradi huu unalenga kuboresha Sera, Sheria, na Kanuni za TEHAMA; kuchochea uunganishaji wa taasisi za Serikali katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; na kuchochea usajili na matumizi ya Huduma za Mawasiliano kwa wanawake. Kwa asilimia kubwa, mradi huu umefanikiwa katika utekelezaji wa malengo yake nchini.
Waziri Silaa pia amesisitiza kuwa kufanikiwa kwa mradi huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kufanikisha mkakati wa Uchumi wa Tanzania ya Kidijitali. Na kwamba Umoja huo umefurahishwa na maendeleo mbalimbali ya kidijitali nchini na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala ya TEHAMA.
Post a Comment