TASAC YATHIBITISHA KUZAMA KWA MELI YA MV. HANIM KILWA MASOKO

****

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limethibitisha kuzama kwa meli ya mizigo ya MV. HANIM yenye namba za usajili 100326 ikiwa imeegeshwa katika fukwe ya Bandari ya Kilwa Masoko (beached) leo tarehe 27 Disemba 2024. Meli hiyo ilisajiliwa Zanzibar tarehe 22 Oktoba, 2024. Ajali hiyo haijasababisha kifo wala majeruhi.

Taarifa ya Jana Desemba 27, 2024 iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu TASAC imeeleza kuwa awali, meli hiyo ilikua kwenye safari yake ya kwanza (maiden voyage), kutokea Bandari ya Mtwara kuelekea Zanzibar, na ina uwezo wa kubeba tani 3,500, lakini ilikua imebeba saruji tani 3,150.

Chanzo cha awali cha ajali ni hitilafu ya kutoboka sehemu ya mwili wa meli (ship hull) upande wa kulia (forward starboard) na kupelekea maji kujaa kwenye matenki ya kuhifadhia maji ya mizania (water stability tanks) yaliyopo upande wa kulia, hivyo kusababisha meli kutitia upande wa kulia (listing to starboard) na kuzama.

TASAC kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri wa Bahari Zanzibar (ZMA) na mamlaka nyingine za Serikali zinaendelea na zoezi la uchunguzi ili kubaini kama kuna chanzo kingine tofauti na kutoboka kwa meli ili kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yoyote aliyesababisha ajali hiyo.

TASAC imetoa rai kwa umma kuzingatia Sheria, Kanuni, Miongozo na Taratibu za Uendeshaji wa Vyombo vya Usafiri Majini hasa katika ununuzi wa meli zilizotumika kuzingatia umri wa meli husika tangu kuundwa kwake, kufanya ukaguzi wa injini na mwili wa meli (Engine and Ship Bottom Survey), pamoja na kujua mizania na uimara wa meli (Stability and Inclining Test) kabla ya kununua na kusajili meli hizo nchini kwa lengo la kulinda maisha ya watu na mali zao.

“Ukiona ukiukwaji wa taratibu za kiusalama na kwa msaada wakati wa dharura tafadhali toa taarifa kwenye kituo cha Kuratibu Utafutaji na Uokoaji (MRCC) kupitia namba za bure 080011 0101 au 0800110107 au barua pepe: mrccdar@tasac.go.tz. Huduma hii inapatikana bure masaa 24 siku zote za wiki.”——imesema taarifa hiyo
 

0/Post a Comment/Comments