TCRA YARIDHISHWA NA TORCH MEDIA,YAIPATIA LESENI YA RUNINGA

 



........................

Na Waandishi wetu,Dar es Salaam/Geita 

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), imeridhishwa na maudhui yanayo rushwa na mtandao wa kijamii wa "Torch Media" na kuipatia leseni ya kurusha maudhui kupitia runinga ya mtandaoni.

Kutokana na leseni hiyo, Torch Media sasa itaanza kurusha maudhui hayo wakati wowote kwa lengo la kuhabarisha jamii, kuelimisha na kuburudisha.

Kwa mujibu wa leseni hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dkt. Jabiri Bakari, Torch Media itaendelea kurusha maudhui ya mtandaoni kwa kipindi cha miaka mitatu.

Aidha, maelekezo hayo yanazingatia kifungu cha Sheria cha 2(a), 4(1) na 23(1)(c) cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, sura ya 306 ya Sheria za Tanzania na sehemu ya 6 ya Udhibiti wa Mawasiliano ya Tanzania.

Sambamba na Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano, sura namba 172 R.E ya Sheria za Tanzania na Kanuni ya 4 ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Kanuni ya mwaka 2018.

"Mwenye leseni atazingatia masharti yote yaliyoainishwa katika leseni hii na udhibiti mwingine mahitaji yaliyotolewa chini ya Kanuni na Kanuni zilizotolewa chini ya Sheria."

"Kadhalika, kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya ufikiaji wowote wa maudhui ambayo ni hatari kwa ustawi wao" imeelezwa na sehemu ya leseni hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Torch Media, James Salvatory Gerald, ameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kuupatia leseni mtandao wa Torch Media kurusha maudhui ya runinga.

"Nimatumaini yetu Watanzania wataendelea kufurahia habari mbalimbali hasa za kijamii kutoka maeneo mbalimbali ya nchi."

"Leseni hii ni chachu kubwa kwetu Torch Media kwa maana tunakwenda kufanya mapinduzi makubwa ya kihabari ili kuhakikisha wasomaji wetu wanapata habari bora zenye ukweli, usahihi na ulinganifu kwa maslahi mapana ya umma."

"Tunaipongeza sana Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano nchini kwa kuona umuhimu wa kutupa leseni mpya ya kurusha habari kupitia runinga ya mtandaoni kwa kuzingatia masharti mbalimbali, hakika tutaendelea kuheshimu mipaka yetu ya kihabari kwa kulinda maadili ya uandishi wa habari," ameongeza Salvatory.

Hata hivyo, ameziomba mamlaka za Serikali kutoa ushirikiano mkubwa kwa waandishi wa habari wa mtandao wa Torch Media ambao wametapakaa sehemu mbalimbali za nchi, kwa kuwapa taarifa muhimu na kwa wakati kwa manufaa mapana ya nchi.

"Nitumie nafasi hii kuziomba mamlaka mbalimbali za nchi kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa waandishi wa habari nchini wakiwemo wa mtandao wetu ili kuihabarisha na kuelimisha jamii mambo muhimu yenye maslahi kwa umma."

"Leseni hii haitakuwa na maana yoyote iwapo umma hautapata habari zenye ubora unaotakiwa, hivyo niwaombe wadau mbalimbali watupe ushirikiano mkubwa katika kutimiza majukumu yetu jambo litakalo saidia jamii kupata maendeleo yanayo kusudiwa," amesema Salvatory.

Mbali na hilo, amesisitiza jamii kutumia mtandao wa Torch Media kufikisha changamoto zao sehemu zinazohusika ili ziweze kipatiwa majibu ya haraka na Serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo badala ya kulalamika na kujichukulia sheria mkononi kinyume na sheria za nchi.

 


0/Post a Comment/Comments