****
MKUU wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Ali Mohamed Shein, amewataka
wahitimu wa chuo hicho kutochagua kazi wanapoingia katika soko la ajira, huku
akiwakumbusha kwamba mafanikio yao kielimu yanaakisi uwezo na nafasi yao ya
kufanikiwa kimaisha hata katika mifumo isiyo rasmi ya ajira.
Hayo yamesemwa na Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Chuo Kikuu
Mzumbe , Dkt. Ali Mohamed Shein wakati wa Mahafali ya 23 ya Chuo Kikuu Mzumbe,
Kampasi ya Dar es Salaam, yaliyofanyika leo Desemba 5, 2024 katika Kituo Cha
Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mahafi hayo, Dkt. Shein amesema kusoma ni
njia moja katika kutafuta maisha, na kwamba hakuna njia ya mkato katika
mchakato huo, huku akiwapongeza kwa mafanikio waliyoyapata katika hatua hiyo
kielimu na kuwatakia kila la kheiri wanapoingia katika hatua ya tatu ya
ushindani kwenye soko la ajira.
“Kusoma ni njia miongoni mwa njia katika kutafuta maisha na
katika hilo hakuna njia ya mkato, nyie mshavuka katika hatua ya kwanza na ya
pili kielimu na sasa mnaingia hatua ya tatu. Elimu haina mwisho, leo
nawapongeza kwa juhudi kubwa, mmehangaika kusoma na hatimaye mmeweza.
“Jitihada kubwa mmeonesha kuwa mnaweza kujipambania na hiyo ni
uthibitisho kwamba mnaweza kujipambania nje ya vyuo, manweza kujipambania
katika soko la ushindani wa ajira, wito wangu kwenu ni kwamba msichague kazi,
msisubiri kuajiriwa serikalini, tumieni elimu kujiajiri.
Katika hotuba yake kwenye mahafali hayo, Mwenyekiti wa Baraza la
Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Saida Yahya-Othman, amewapongeza wafanyakazi wa chuo
kwa kazi kubwa na adhimu wanayoendelea kuifanya ya kuwaandaa vijana, na kwamba
anaamini wanaohitimu hao wako tayari kuikabili dunia na changamoto zake.
Prof. Saida amesema “Niwapongeze wahitimu wote mtakaotunukiwa
Stashahada, Astashahada na Shahada leo, juhudi na uvumilivu mliouonesha kipindi
chote cha masomo yenu, hakika zinawastahilisha vyeti mnavyopokea leo.
“Tunaposherehekea mafanikio ya kuhitimu masomo yetu, tufanye
tafakuri ya maisha yetu ya chuoni na yale ya baadae, na changamoto
zitazotukabili katika soko la ajira, na katika maisha yetu kwa ujumla.
Changamoto ni nyingi, na zimeathiri kwa kiasi kikubwa mfumo wa kiutendaji na
ajira.
Post a Comment