*******
Na Daniel Limbe,Chato
“Jenga ndoto zako wewe mwenyewe, la sivyo mtu mwingine atakuajiri kujenga zake.”
Maneno hayo yamekuwa na maana kubwa sana katika jamii na taasisi yoyote yenye kutaka mafanikio katika mipango iliyojiwekea ili kutekeleza matamanio yake kwa ufanisi na kuziishi ndoto hizo.
Kutokana na ukweli huo,Chama cha kuweka na kukopa cha walimu Chato(Chato Teachers saccos) kimewataka wanachama wake kuwa waaminifu katika kulipa mikopo waliyokopeshwa ili kukinusuru kufilisika.
Ni kutokana na zaidi ya milioni 69 ambazo bado zipo mikononi mwa wanachama waliokopa kwa muda mrefu na kushindwa kulipa kwa wakati licha ya kusaini mikataba ya kulipa pasipo usumbufu.
Mbali na wanachama hao,zaidi ya milioni sita zinadaiwa kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo,deni ambalo limekuwa chefuchefu kutokana na kutolipwa kwa wakati kinyume na makubaliano ya mwajili huyo.
Hayo yamebainishwa na mwenyekiti wa Chama hicho,Petro Rwegasira,ambaye amesema kutolipwa madeni kwa wakati kunadhoofisha ufanisi wa taasisi hiyo ambayo imekuwa mkombozi kwa watumishi wengi wa wilaya hiyo, ukilinganisha na taasisi zingine za fedha ambazo hukopesha kwa masharti magumu.
Mbali na masharti hayo, baadhi ya taasisi zimekuwa zikiwadhalilisha wanaposhindwa kulipa mikopo yao kwa wakati hali inayopunguza mwamko wa kutimiza majukumu yao kazini kutokana na msongo wa mawazo.
Meneja wa taasisi hiyo,Pius Katani,mbali na kujivunia hati safi katika ukaguzi wa fedha za taasisi hiyo, amesema wanajiandaa kuendesha ushirika huo kidijitali kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji ikiwa ni pamoja na kushusha kiwango cha makato ya mikopo kwa wakopaji.
Amesema taasisi hiyo ina fedha za kutosha na kwamba imepiga hatua kubwa za kimaendeleo kutoka kwenye utegemezi wa kukopa mtaji kwenye benki za biashara hadi kujitegemea kwa mtaji wake na kwamba wamefanikiwa kujenga ofisi ya kisasa ambayo itaanza kutumika mapema mwaka 2025.
Akizungumzia ripoti ya ukaguzi wa fedha za Saccos hiyo,Mkaguzi kutoka shirika la ukaguzi na usimamizi wa vyama vya ushirika(Coasco) Kagera,Michael Kireo,amesema chama hicho kimefanikiwa kupata hati safi na kwamba kinajiendesha vizuri isipokuwa juhudi ziongezwe kwenye ukusanyaji madeni ili kukuza mtaji wa taasisi hiyo.
"Lengo kuu la taarifa ya ukaguzi ni kuwajulisha wanachama hali halisi ya uhai wa chama chao na jinsi kinavyojiendesha" amesema Kireo.
Kutokana na hali hiyo,mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) wilaya ya Chato,Barnabas Nyerembe,ameahidi kuzungumza na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo ili kuongeza msukumo wa kumtaka kulipa fedha anazodaiwa na taasisi hiyo,kwa kuwa ilani ya Chama hicho imeahidi kuimalisha vyama vya kuweka na kukopa(Saccos).
Baadhi ya wanachama wa Chato Teachers Saccos wakiendelea na mkutano wao mkuuAliyesimama ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Chato,Barnabas Nyerembe
Mwisho
Post a Comment