Waziri wa Maliasili na
Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amekabidhi Malori matano (5) na
mitambo mitano (5) yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 2.4 sawa na
trakibani Shilingi Bilioni 6.4 za Kitanzania viliyonunuliwa kupitia mradi wa
Dharura kwa Uhifadhi na Utalii Tanzania (Emergency and Recovery Support for
Biodiversity in Tanzania) kupitia benki ya maendeleo ya Ujerumani (KfW).
Akizungumza katika
makabidhiano hayo, Jana Desemba 2, 2024 katika ukumbi wa Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (Mpingo House) jijini Dar es Salaam, Mhe. Chana alisema kuwa
vifaa hivyo vitaenda kusaidia shughuli za Uhifadhi pamoja na kuboresha
miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, Nyerere na Pori la Akiba Selous
kwa malengo ya kupunguza athari zilizosababishwa na janga la UVIKO-19 kwenye
Utalii na Uhifadhi.
Kufuatia hatua hiyo, Chana aliiagiza Bodi na Wakuu wa Mashirika ya
TANAPA na TAWA kuhakikisha vitendea kazi hivyo vinatumika kufanya kazi
zilizokusudiwa za Uhifadhi wa Maliasili na Utalii na kutunzwa ipasavyo kwa
mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu za matumizi ya vifaa vya Serikali.
Naye, Mwenyekiti wa
Bodi ya Wadhamini TANAPA, Jenerali Msaafu George Waitara aliipongeza Serikali
ya Ujerumani kwa kuendelea kusaidia uhifadhi nchini Tanzania hasa katika miradi
ya dharura.
“Msaada huu wa dharura
umetuwezesha kuvuka kipindi cha dharura cha UVIKO- 19 kwa kazi za Uhifadhi
kuendelea bila kuyumba kwenye mifumo ya kiikolojia, kutumika kuboresha na
kuimarisha juhudi za uhifadhi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”
amesisitiza.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mkazi wa Frankfurt Zoological Society (FZS), Dkt Ezekiel Dembe )
alisema kuwa Frankfurt Zoological Society imekuwa Tanzania kwa zaidi ya
miaka 65 na kwamba inajivumia kufanya kazi na Wizara ya Maliasili na Utalii,
TANAPA, TAWA na wadau wengine kwa sababu wamekuwa wakitekeleza makubaliano ya
mikataba ipasavyo.
Mradi wa Usaidizi wa dharura kwa Uhifadhi na Utalii nchini Tanzania umesaidia juhudi za kutoa msaada wa haraka na mipango ya muda mrefu ya kurejesha na kulinda mifumo ikolojia mbalimbali ya Tanzania, hasa pale ambapo vitisho vikubwa kama mabadiliko ya tabianchi, ujangili, au majanga ya asili yanayosababisha uharibifu kwa wanyamapori na makazi yao, juhudi za mradi zinahusisha ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania na Ujerumani, Shirika la Frankfurt Zoological Society pamoja na jamii za wenyeji ili kudhibiti na kuimarisha ustahimilivu wa bioanuwai nchini.
Post a Comment