WAZIRI JAFO AAGIZA KUTATULIWA CHANGAMOTO ZA KISHERIA ZINAZO ZUIA USHINDANI

********

Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo, amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara kuwasilisha changamoto zote za kisheria na kanuni zinazozuia wafanyabiashara kushiriki kikamilifu katika ushindani, ili zitafutiwe ufumbuzi na kuimarisha sekta ya biashara nchini.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Ushindani Duniani, Waziri Jafo alisema serikali ya awamu ya sita inajitahidi kuboresha miundombinu ili kukuza ushindani wa bidhaa katika masoko ya kitaifa. Alisisitiza kuwa mijadala ya maadhimisho hayo iwasilishwe kwake ndani ya siku 14 ili kutekeleza mawazo yaliyopendekezwa kwa lengo la kukuza biashara na ushindani wa bidhaa.

Waziri Jafo pia alimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) kuharakisha michakato ya maunganiko ya kampuni, ili kutoa fursa kwa vijana wa Kitanzania, hasa wale wanaomaliza vyuo vikuu, kupata ajira. Alihimiza makampuni kuongeza kasi ya uwekezaji na ushirikiano ili kuchochea uchumi na kutoa ajira.

Aidha, alisema maadhimisho hayo yataleta fursa za kujifunza kuhusu masuala ya kisheria na kikanuni yanayohusiana na ushindani, huku akiwataka vijana kuhakikisha wanatumia juhudi na maarifa katika sekta ya viwanda na biashara.

Mwenyekiti wa Tume ya FCC, Dkt. Aggrey Mlimuka, alisema tume hiyo inahakikisha fursa sawa kwa washindani wakubwa na wadogo, huku Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, alieleza kuwa maadhimisho haya ni ya kwanza tangu marekebisho ya sheria nchini, na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha mageuzi hayo.

Maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani hufanyika kila mwaka tarehe 5 Desemba, na kaulimbiu ya mwaka huu ni "Sera ya Ushindani na Kudhibiti Kukosekana kwa Usawa Katika Uchumi".

 Mwenyekiti wa Bodi Tume ya Ushindani (FCC) Dkt. Aggrey Mlimuka  akizungumza jambo leo Disemba 5, 2024 jijini Dar es Salaam katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Ushindani Duniani ambayo yamebeba kauli mbiu “Sera ya ushindani na kudhibiti kukosekana kwa usawa katika uchumi” 
 Mkurugenzi Mkuu wa  Tume ya Ushindani (FCC) William Erio  akizungumza jambo leo Disemba 5, 2024 jijini Dar es Salaam katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Ushindani Duniani ambayo yamebeba kauli mbiu “Sera ya ushindani na kudhibiti kukosekana kwa usawa katika uchumi” 

0/Post a Comment/Comments