Na Daniel Limbe, Chato
MKAZI wa kitongoji cha Mpakani,kijiji cha Mkuyuni wilayani Chato mkoani Geita,Juma Ndahosigae(51) amekufa maji baada ya kujitumbukiza ndani ya ziwa Victoria kutokana na kiwewe.
Kabla ya kufikwa na umauti huo alikuwa akidai anaona baadhi ya watu wakitaka kumuua kwa mapanga na mikuki hasa nyakati za usiku huku taarifa hizo akiziwasilisha kwa mjumbe wa nyumba kumi wa eneo hilo.
Akizungumza na vyombo vya habari,mke wa marehemu huyo, Faines Philipo(51) amesema mumewe amefariki kwa kujitumbukiza kwenye maji ndani ya ziwa viktoria majira ya saa 10 jioni hali iliyosababisha umauti wake.
Amesema licha ya mume wake kuwa na historia ya unywaji wa pombe kupindukia pamoja na ugonjwa wa kifafa ulioibuka katika umri wa utu uzima, changamoto nyingine iliyoibuka na kumsababishia kifo ni kiwewe cha kuona vitu vibaya pasipo wengine kuviona.
"Mume wangu alikuwa akilalamika mara kwa mara kuona watu wabaya (washirikina) wakitaka kumuua kiasi kwamba wakati mwingine alikuwa analazimika kwenda kulala kwa jirani anapokuwa pekee yake nyumbani".
"Zipo nyakati ambazo alikuwa akipiga kelele usiku tukiwa tumelala pamoja na ukimuuliza anasema anaona watu wanataka kumuua na baadhi yao alikuwa akiwataja kwa majina na tunawafahamu" amesema Faines.
Kwa upande wake mkwe wa marehemu(mke wa mtoto wa marehemu) Wema Pius(25) amesema kabla ya umauti marehemu aliomba kupewa chakula na akaketi chakulani na mjukuu wake na baada ya kumaliza chakula alitoka nyumbani hapo kwa kukimbia kuelekea ziwani kujitumbukiza.
Takribani dakika 10 alipewa taarifa na jirani yake kuwa baba mwenye nyumba amekatiza barabara kuelekea ziwani lakini akiwa anakimbia,hali iliyo wasababisha kumfuatilia ili kujua kilichomsibu.
Anasema baada ya kushindwa kufika ufukweni kutokana na tope nyingi zilizopo njiani,walilazimika kurejea nyumbani umbali wa mita 100 kutoka ziwani hapo, ambapo walipuliza kipenga ili kuomba msaada kwa wananchi ambao walifika haraka na kushirikiana katika uokozi.
Kwa upande wake jirani wa marehemu,Charles Luyuga, amekiri kumshuhudia marehemu akielekea ziwani na kulazimika kumfuatilia ili kunusuru maisha yake lakini jitihada hizo ziligonga mwamba baada ya wananchi kumuopoa akiwa tayari amepoteza maisha.
Mjumbe wa nyumba kumi(Balozi) Sevelina Gerald,amethibitisha kupokea malalamiko ya mwananchi huyo kuona baadhi ya watu wanaotishia kumuua wakati wa usiku na wakati mwingine chakula chake kupotea katika mazingira ya kutatanisha kabla ya kukila.
" Ni kweli kabisa alikatiza barabara hapa akiwa anakimbia kuelekea ziwani na haraka nilimuita mke wa mtoto nikamuuliza kulikoni,naye akabaki anashangaa kwa sababu alimwandalia chakula nje akiwa na mjukuu wake, kisha yeye akaingia ndani ya nyumba kuendelea na majukumu mengine"amesema
"Baada ya kuwa tumepata shaka ya tukio hilo na baada ya sisi kushindwa kufika ziwani ilibidi kupuliza kipenga haraka ambapo wananchi walikusanyika na kuanza kumtafuta ndani ya maji, na ilipofika majira ya saa 11:30 tulifanikiwa kumpata akiwa amekufa maji"amesema Luyuga.
Mkuu wa jeshi la Zima moto na uokoaji wilaya ya Chato, Inspekta Ramadhan Maneno,amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba walifika eneo la tukio na kukuta wananchi wameshaopoa mwili huo.
"Ni kweli mtu huyo alikufa maji na sisi Jeshi la zimamoto na uokoaji tulifika na kukuta wananchi tayari wameshamuopoa ndani ya ziwa,na tuliuchukua mwili huo na kuupeleka chumba cha kuhifadhia maiti kwaajili ya taratibu zingine za kipolisi" amesema Maneno
Post a Comment