****
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila leo Januari 17,2025 amefika katika kiwanda cha Saruji Wazo Hill Wilaya ya Kinondoni kwa lengo la kujionea malalamiko ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakitolewa na uongozi wa kiwanda hicho.
RC Chalamila amesema malalamiko hayo ni kama uvamizi wa eneo la kiwanda ambao umepelekea kiwanda kuwa na eneo dogo licha ya kuwa na eneo kubwa hapo awali pia mifumo ya upatikanaji wa maji toshelevu kwa matumizi ya kiwanda.
Aidha katika kufikia suluhu ya malalamiko hayo RC Chalamila amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kuitisha mkutano wiki ijayo ambao utajumuisha wananchi wa eneo hilo, uongozi wa Mkoa na Wilaya pamoja na uongozi wa kiwanda ili kuanza upya mazungumzo, pia amemtaka Mtendaji mkuu DAWASA kufika mara moja katika kiwanda hicho kuketi na menejimenti ya kiwanda hicho ili kuona namna bora ya kumaliza changamoto hiyo.
Vilevile Chalamila amemuagiza Naibu kamisha wa Ardhi Mkoa kwa kushirikiana na wanasheria chini ya usimamizi wa Katibu Tawala wa Mkoa kuunda kamati ndogo ambayo itapitia malalamiko na hukumu zilizotolewa na mahakama katika eneo hilo ili kuweza kumshauri Mkuu wa Mkoa njia sahihi za kupita kwa lengo la kupunguza malalamiko kwa mwekezaji.
Sanjari na hilo RC Chalamila amesema Kiwanda hicho ni muhimu sana kwa masilahi mapana ya umma kwa kuwa kinatoa fursa kubwa ya ajira lakini pia huchangia katika pato la Taifa.
Post a Comment