******
Na Daniel Limbe,Chato
KUELEKEA Uchaguzi mkuu wa rais wabunge na madiwani nchini,serikali, viongozi wa dini,waumini pamoja na wananchi wa wilaya ya Chato mkoani Geita,wameungana pamoja kuliombea Taifa amani huku Diwani wa kata ya Chato akikumbushia ahadi ya rais ya mkoa mpya wa Chato.
Maombezi hayo yamefanyika leo Januari 30,2025 kwenye viwanja vya stendi ya zamani Chato mjini na kuwakusanya viongozi mbalimbali wa dini ya Kikristo na Kiislam kutoka pande zote za wilaya hiyo huku wakimwomba mwenyezi Mungu kuivusha nchi salama kabla na baada ya Uchaguzi mkuu kumalizika.
Awali Diwani wa kata ya Chato, Mange Ludomya, mbali na kuwataka watanzania kuendelea kuliombea taifa amani, amemwomba rais Dkt. Samia Suluhu, kutimiza ahadi yake aliyoitoa machi 26,2021 wakati wa mazishi ya mtangulizi wake Hayati rais Dk. John Pombe Magufuli, ya kutimiza ndoto za wilaya hiyo kupewa hadhi ya mkoa.
Aidha amesema faraja kubwa ya wananchi wa wilaya hiyo ni kuona rais Samia akitekeleza miradi iliyokwama baada ya kifo cha Hayati Magufuli ikiwemo,ujenzi wa Chuo kikuu tawi la UDSM kilichokusudiwa kujengwa kwenye kijiji cha Kasagara pamoja na ukamilishaji msikiti wa Ijumaa ulionzishwa na mtangulizi wake.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa kamati ya amani wilaya ya Chato,ambaye pia ni shekhe mkuu wa wilaya hiyo,Abdulrahiman Ismail, amesema amani,haki na maridhiano ndiyo msingi mkuu wa utulivu na kichocheo cha maendeleo katika nchi yoyote duniani.
Kauli hiyo inaungwa mkono na nukuu ya mwana falsafa Chinua Achebe "Tuendeleze mambo ambayo yanaweza kutuunganisha pamoja kuliko mambo ambayo yatasababisha kutengana"
Shekhe Abdulrahiman,amesema ni muhimu kwa wananchi wote kuomba amani ya taifa ili Mwenyezi Mungu akaiepushe nchi kutokea machafuko, majanga na magonjwa mbalimbali ambayo ni hatari kwa wananchi na Tanzania kwa ujumla.
"Muhimu tukumbuke kuwa katika changuzi ndipo hutokea machafuko katika nchi mbalimbali na kwamba ili kujinusuru katika kadhia hiyo ni kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika kila jambo jema"amesema.
Vile vile ameipongeza serikali kuendelea kusimama kidete katika kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umeongeza chachu ya amani upendo na maridhiano ya kitaifa.
Mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura,ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo,Martine Shigela, amesema Tanzania inaendelea kujivunia amani iliyopo kutokana na misingi mizuri iliyoasisiwa na viongozi wakuu wa nchi kuanzia utawala wa awamu ya kwanza wa Hayati rais Mwl. Julius Kambarage Nyerere,Ally Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa,Jakaya Mrisho Kikwete,John Pombe Magufuli na sasa Samia Suluhu Hassan.
Amesema tofauti na nchi zingine Tanzania ilijipatia uhuru wake kwa amani pasipo kumwaga damu kutokana na wananchi kumtanguliza mbele Mungu kwa njia ya maombi badala ya kutumia silaha.
Pamoja na mambo mengine amesema Tanzania inaelekea katika Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kwamba kipindi kama hicho hutokea vurugu na mambo mbalimbali yasiyofaa,hivyo ni muhimu kwa watanzania kuendelea kuliombea taifa ili Mwenyezi Mungu aivushe nchi salama.
"Rai yangu kwenu ni kuendeleza utamaduni wetu wa kuishi kwa amani na upendo,tujiepushe na vurugu na machafuko mbalimbali,wanasiasa wote tuwaombee wakaendeshe siasa zao kwa ustaarabu badala ya kutumia matusi na kauli zisizofaa kwa nchi yetu" amesema.
Aidha katika mkutano huo, Bura ametangaza kiasi cha sh. 2,000,000 zilizotolewa na rais Samia katika kuunga mkono jitihada za viongozi hao wa dini kuliombea taifa,huku mkuu wa mkoa huo akichangia sh.500,000 na mkuu wa wilaya hiyo akichangia sh. 200,000.
Kwa upande wake Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mlimani Chato, Padri Edmund Revelian, amesema watanzania hawana budi kuliombea taifa kwa wema na kwamba kwa kila jambo lolote gumu kwa wanadamu tumkabidhi Mwenyezi Mungu aweze kutenda.
"Lile unaloliweza kutenda litende kwa wema, na usiloliweza mwachie Mungu atende"amesema.
Mchungaji wa Kanisa la kiinjili la kirutheli Tanzania(KKKT) usharika wa Chato, Justine Mutayabarwa, amesema iwapo watanzania watajinyenyekeza kwa Mwenyezi Mungu katika kutafuta amani ya nchi hakika Mungu atajibu maombi yao badala ya kutumia akili za kibinadamu.
Katika hatua nyingine, wananchi na viongozi mbalimbali katika mkutano huo wamemchangia rais Samia Suluhu Hassan kiasi Cha shilingi 1,430,000 kwaajili ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM).
Mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura,akizungumza katika mkutano wa maombi.Viongozi mbalimbali wa Dini wakiwa wameketi wakiendelea kuliombea taifaWananchi mbalimbali wakiendelea na maombi kwaajili ya taifa.
Mwisho.
Post a Comment