*****
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Evaristo Liwa, amesema chuo hicho kimewezesha wanafunzi kuwa na ustadi wa hali ya juu ili waweze kushindana kwenye soko la ajira.
Profesa Liwa alieleza kuwa soko la ajira la sasa linahitaji watu wenye ujuzi mkubwa kutokana na ushindani mkubwa uliopo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kusaini makubaliano ya kuanzisha programu ya Generation Empower, Profesa Liwa alisema mradi huo utawanufaisha wanafunzi wa mwaka wa mwisho kwa kuongeza ujuzi wao ili waweze kushindana katika soko la ajira.
“Mradi huu unalenga kuimarisha ujuzi wa vijana wetu na kutatua changamoto za ushindani kwenye soko la ajira. Kama chuo, tunataka kuendeleza ubora wa elimu na hii ni fursa nzuri kwa wanafunzi wetu,” alisema Profesa Liwa.
Ameongeza kuwa wanafunzi watajengewa uwezo wa kuwa viongozi bora na wasuluhishaji wa migogoro, hasa ile inayohusiana na ardhi, akisisitiza umuhimu wa kujiamini, iwe kwa mtu anayeajiriwa au anayejiajiri.
“Serikali inataka wanafunzi wawe na ujuzi wa kusuluhisha migogoro ya jamii. Wanafunzi wa Ardhi wanapaswa kuelewa namna bora ya kutoa maelekezo na kuzungumza kwenye hali ya migogoro,” alisema.
Pia, Profesa Liwa alisisitiza umuhimu wa elimu ya fedha kwa wanafunzi, kwani elimu hiyo ni muhimu kwa kila mtu, si tu kwa wanafunzi bali kwa jamii nzima.
Post a Comment