Meneja wa Benk ya CRDB Kanda ya magharibi,Jumanne Wambura,akizungumza na wazazi,walimu na wanafunzi waliojitokeza kwenye hafra ya kukabidhi madawati.
******
Na Daniel Limbe,Chato
BENKI ya CRDB imetoa msaada wa madawati 40 yenye thamani ya takribani milioni 3.5 kwenye shule ya msingi Mkuyuni wilayani Chato mkoani Geita ikiwa ni kuunga mkono jitihada za serikali katika uboreshaji wa elimu kwa jamii.
Licha ya shule hiyo kuwa na miundombinu bora ya madarasa imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa madawati na kusababisha baadhi ya watoto kukaa chini, hivyo kusababisha kutofanya vizuri katika masomo yao.
Kutokana na hali hiyo,Benki ya CRDB tawi la Chato ikaamua kujitosa kusaidia kutatua changamoto hiyo kwa lengo la kuinua taaluma kwa wanafunzi sambamba na kuhamasisha utunzaji wa mazingira ili kuboresha afya za watoto hao.
Akizungumza katika hafra ya kukabidhi madawati hayo,Meneja wa CRDB Kanda ya magharibi, Jumanne Wambura, amesema msaada huo umetokana na benki hiyo kutenga kiasi cha asilimia moja ya faida yake iliyopatikana kwa kipindi cha mwaka mmoja na kwamba jamii haina budi kuendelea kutumia huduma za benki hiyo ili kuiwezesha kusaidia katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
"Ni utaratibu wetu wa kutenga kiasi cha asilimia moja ya faida tunayoipata kwa mwaka kuchangia maendeleo ya wananchi japo siyo maeneo yote,ninyi Chato mmepata bahati hii na tuna ahidi kuendelea kusaidia zaidi ya hapa isipokuwa muendelee kutuunga mkono kwa kutumia huduma za kifedha kupitia benki yetu pendwa ya CRDB" amesema Wambura.
Aidha amesema amepokea kwa mikono miwili maombi ya mkuu wa wilaya hiyo,kuitaka Benk ya CRDB kushirikiana na taasisi zingine binafsi na za umma ikiwemo wakala wa misitu mchumi(TFS) wilaya ya Chato kutatua uhaba wa madawati zaidi ya 20,000 yanayohitajika kwenye wilaya hiyo.
Awali mwalimu mkuu wa shule hiyo,Verena Nicholaus, mbali na kuishukuru benki ya CRDB kwa msaada huo,amesema shule yake bado inakabiliwa na uhaba wa madawati takribani 200 kutokana na ongezeko la wanafunzi walioandikishwa kuanza darasa la awali na msingi kwa mhula wa masomo wa mwaka 2025.
Kadhalika amesema kukosekana kwa madawati imekuwa ikisababisha baadhi ya watoto kutojifunza vizuri na wengine kuwa na mwandiko mbaya jambo linaloathiri ubora wa taaluma.
Kutokana na kauli hiyo, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chato,Christian Manunga, akalazimika kuiagiza Ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo kutoa mbao takribani 100 ili ziweze kuondoa kabisa changamoto ya madawati kwenye shule hiyo huku akiiomba CRDB kusaidia vyuma ili kukamilisha dawati hizo kwa ubora zaidi.
"Nimeisikiliza vizuri taarifa fupi ya shule hasa katika uhaba wa madawati, niwapongeze sana wadau wetu wa CRDB kwa kutuunga mkono,sasa nikuagize kaimu mkurugenzi hakikisha halmashauri inapata mbao kuanzia 100 na CRDB mtusaidie kupata vyuma ili tuondoe kabisa changamoto ya madawati kwenye shule hiyo kabla ya februari 5 mwaka huu"amesema Manunga.
Mkuu wa wilaya hiyo,Louis Bura, ametumia fursa hiyo kuzitaka taasisi zingine kuguswa na kadhia ya uhaba wa madawati kwenye wilaya hiyo,na kwamba jitihada zilizofanywa na Benk ya CRDB zinapaswa kuungwa mkono na jamii yote ikiwa ni pamoja na kufanya miamala ya kifedha kupitia taasisi hiyo kwa kuwa imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada za serikali.
Amewataka walimu na wanafunzi wa shule hiyo,kuyatunza madawati yaliyotolewa na wahisani hao kwa lengo la kusaidia kuboresha taaluma kwa muda mrefu.
Vilevile ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kuinua uchumi wao badala ya kukaa vijiweni na kulalamikia serikali, na kwamba huku akisisitiza kuwa heshima ya mwanaume ni kuwa na pesa.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wake, mwenyekiti wa kijiji hicho,Goodluck Phinias,amesema shule hiyo imekuwa ni tegemeo kubwa la wananchi licha ya kuwepo kwa changamoto ya miundo mbinu ya barabara kufika shuleni hapo hasa kipindi cha mvua za masika.
Ameiomba serikali kutatua kero hiyo kwa kujenga barabara,madaraja na kutengeneza mtalo mkubwa wa maji utakao kuwa suluhisho la shule hiyo kukumbwa na mafuriko na kusababisha wanafunzi kukosa vipindi vya masomo shuleni hapo.
Kulia ni mkuu wa wilaya ya Chato, Louis Bura akipongezana na Meneja wa CRDB Kanda ya magharibi,Jumanne Wambura aliyeko kushoto.
Post a Comment