.............
Na Daniel Limbe,Chato
OFISI ya mkuu wa wilaya ya Chato mkoani Geita kwa kushirikiana na wananchi wa wilaya hiyo wamemtakia heri ya kumbukizi ya kuzaliwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni pamoja na kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kadhalika wamempongeza Dkt. Hussein Mwinyi, kuteuliwa na Chama hicho kuwa mgombea wa nafasi ya urais katika serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa wilaya ya Chato, Louis Bura,wakati akizungumza na waandishi wa habari ofsini kwake,ambapo amewatakia maisha marefu,afya njema, hekima na busara katika kuwatumikia watanzania.
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya hiyo, Januari 27,2025 ni kumbukizi ya kuzaliwa kwa Rais Dkt. Samia na kwamba Ofisi yake imewiwa kumtakia kila la heri katika utumishi wake uliotukuka kutokana na maendeleo makubwa yanayoendelea kupatikana baada ya kupokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake,Hayati rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Aidha Bura,amesema wananchi wa wilaya ya Chato wanayo imani kubwa rais Samia na kwamba wanaendelea kumuunga mkono katika jitihada zake za kuwaletea maendeleo wananchi.
"Tunamtakia afya njema,hekima busara na maarifa ya kuwatumikia watanzania na kwamba sisi wananchi wa wilaya ya Chato tutaendelea kumuunga mkono katika hatua zote anazofanya ili kuhakikisha Taifa letu linapiga hatua kubwa katika maendeleo" amesema Bura.
Mwisho.
Post a Comment