SERIKALI imesema usaili wa kada za Ualimu utaendeshwa na
Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa kushirikiana
na Ofisi ya Rais (UTUMISHI); Ofisi ya Rais (TAMISEMI); Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia; Wizara ya Afya; Tume ya Utumishi wa Walimu; Ofisi za Wakuu wa
Mikoa yote na wataalamu mbalimbali kutoka katika Taasisi za Umma.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George
Simbachawene katika mkutano na wanahabari ofisini kwake Mtumba ambapoa amesema usaili
utaanza Kuanzia tarehe 14 Januari hadi terehe 24 Februari, 2025,
Simbachawene amesema usaili huo una lengo la
kujaza nafasi elfu kumi na nne mia sita na arobaini na nane (14,648)
zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kupunguza uhaba wa walimu
nchini.
"Ninapenda kuchukua nafasi hii kuwasihi sana
wale wote walioitwa kwenye usaili wajiandae vyema kwa usaili huo kwani nafasi
hizi ni za ushindani."
Waziri huyo amesema kulingana na mahitaji ya elimu
kwa sasa, wataajiriwa wataalamu wa fani za Amali.
"Hivyo, nawasihi sana wale wote watakaopata
nafasi ya kuajiriwa, wawe tayari kujiendeleza ili kuweza kukidhi matakwa ya
ajira zao katika Utumishi wa Umma."
Simbachawene amesema kuwa Usaili huo wa kada za Ualimu
utafanyika katika Mkoa ambao kila msailiwa anaishi au aliombea kazi, Lengo kuu
la utaratibu huo ni kuwapunguzia gharama za kusafiri na mambo mengine.
Sekretarieti ya Ajira ilitoa matangazo kumtaka
kila msailiwa kuhuisha taarifa zake katika akaunti yake ya Ajira Portal sehemu
iliyoandikwa ‘current physical adress’ kwani ndipo walipopanguwa vituo vya
usaili kulingana na anuani walizojaza.
"Hivyo, ninawasihi sana waombaji wote
kuhakikisha kila mmoja anakwenda katika kituo ambacho amepangiwa kwa ajili ya
usaili kwani mahitaji yake ya msingi yapo huko."
Aidha Simbachawene amesema usaili wa awali wa
kuandika (Mchujo) kwa kada za Ualimu utafanyika kwa njia ya kuandika kwa mkono
kwa kada zote na ngazi zote za elimu.
Hata hivyo Simbachawene amewakumbusha wale wote
watakaokwenda kwenye usaili wahakikishe wanabeba vyeti vyao Halisi kikiwemo
Cheti cha Taaluma na Cheti cha kuzaliwa.
Vilevile, wasailiwa wanapaswa kwenda na namba zao
za usaili walizotumiwa kwenye akaunti zao za ajira portal pamoja na kuzingatia
Ratiba kama ilivyopangwa na Sekretarieti ya Ajira.
Post a Comment