********
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB)
imeingia makubaliano na Shirika la Ndege la Uturuki kutangaza utalii wa
Tanzania duniani kupitia safari za ndege za shirika hilo.
Makubaliano hayo yamefanyika leo Jumatano Januari 8, 2025 jijini Dar es Salaam,
huku ikielezwa kuwa lengo ni kuongeza idadi ya watalii na wawekezaji katika
sekta hiyo nchini.
Katika hafla ya makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania
(TTB), Ephraim Mafuru amesema wamechagua shirika hilo la ndege kwa sababu lina
idadi ya ndege zaidi ya 490 na linafanya safari zake katika miji zaidi ya 350.
“Kwa Afrika tu, linafanya safari zaidi ya 61, hivyo Tanzania itaweza kutangazwa
vizuri katika hiyo miji yote duniani,” amesema Mafuru.
Ameongeza kuwa matangazo ya vivutio vya utalii vya Tanzania yatakuwa katika
ndege za shirika hilo, tovuti, na ofisi zao zote duniani.
Pia, yatawalenga abiria wenye safari zenye lengo la kutangaza utalii wa
Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Uturuki nchini Tanzania, Kadir
Karaman amesema makubaliano hayo yataimarisha lengo la pamoja la kuifungua
Tanzania kwenye masoko ya utalii ya kimataifa, pia yatakuwa na manufaa kwa
pande zote.
Post a Comment