Na: Dk. Reubeni Lumbagala
Kwa hivi Sasa Giza limepungua vijijini na mijini Hali hii haijatokea kwa bahati mbaya, bali ni matokeo ya utashi wa kisiasa alionao Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na serikali yake nzima katika kuhakikisha wananchi waishio vijijini na mijini wanasambaziwa nishati ya umeme ili giza litoweke kabisa ili kusudi juhudi kubwa za kimaendeleo zinazofanywa na serikali na wadau wengine wa maendeleo ziweze kufanikiwa kwa urahisi kupitia upatikanaji wa umeme.
Katika ulimwengu wa sasa, umeme si anasa bali ni hitaji muhimu katika kuharakisha maendeleo kijamii na kiuchumi kuanzia ngazi ya mtu mmoja mmoja hadi taifa Hivyo basi, kwa kutambua umuhimu huu, juhudi za usambazaji nishati ya umeme zimefanyika kwa kasi kubwa.
Utashi wa Rais Dk. Samia kwenye usambazaji umeme umejidhihirisha kwa kuongeza vyanzo vya uzalishaji umeme, hii imesaidia kuongeza uwezo wa uzalishaji Megawati nyingi ambapo sasa Tanzania inazalisha umeme zaidi ya Megawati 3000 zaidi ya mahitaji yake ambayo ni Megawati 1,800.
Vilevile, Rais Dk. Samia ameiwezesha Wizara ya Nishati raslimali fedha za kutosha kuweza kugharamia utekelezaji wa miradi mingi ya usambazaji wa nishati ya umeme mijini na vijijini, hivyo kuongeza kasi ya usambazaji umeme kwa wakati.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko, kasi ya uzalishaji umeme nchini imeongezeka kutoka Megawati 1470 hadi 3077.
Ndiyo maana hivi sasa upatikanaji wa nishati ya umeme Tanzania ni zaidi ya asilimia 78 huku vijiji vyote 12,318 nchini vikipata umeme, hii ni sawa na usambazaji umeme wa asilimia 100 katika ngazi ya vijiji. Katika ngazi ya vitongoji, vitongoji 36,000 zimeshafikishiwa umeme kati ya vitongoji 64,000 vilivyopo nchini.
Aidha, dhamira ya serikali ni kuhakikisha wateja Milioni 13.5 wanaunganishiwa umeme ifikapo mwaka 2030 kutoka wateja Milioni 5.2 ya sasa.
Mafanikio yaliyopatikana katika mashirikiano na mataifa mengine (Diplomasia) na usambazaji wa nishati ya umeme, yamechangia Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Nishati wa Nchi za Afrika (Africa Energy Summit) ambapo mkutano huo unafanyika nchini kwa siku mbili yaani Januari 27 na 28, 2025 katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam).
Katika mkutano huo, Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) Dkt. Akinumwi Adesina ameipongeza Tanzania Kwa mafanikio makubwa katika usambazaji umeme. "Naomba nitumie fursa hii kumpongeza Rais wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha wananchi wa Tanzania kufikiwa na nishati ya umeme katika vijiji vyote, jambo hili linastahili kupongezwa kutokana na umuhimu wa nishati hii katika maendeleo" amesema Dkt. Adesina.
Mkutano huo umedhamiria kuweka mikakati itakayowezesha Waafrika Milioni 300 waishio Kusini mwa Jangwa la Sahara kupata umeme ifikapo mwaka 2030, hii inatokana na Takwimu zilizopo zinazoonyesha Waafrika Milioni 685 hawana umeme.
Katika Waafrika Milioni 300 wanaotarajiwa kufikishiwa umeme ifikapo mwaka 2030, kati yao ni Watanzania Milioni 13.5 watapata umeme.
Ikumbukwe kuwa usambaji umeme mijini na vijijini utaongeza kasi ya ujenzi wa viwanda, ukuaji wa shughuli za kibiashara na kiuwekezaji, na hivyo kuchagiza ukuaji wa uchumi na maendeleo. Ni muhimu wa wananchi kutumika fursa ya upatikanaji wa nishati ya umeme katika maeneo yao kwa manufaa ya kiuchumi zaidi.



Post a Comment