VIONGOZI WA AFRIKA WAONDOKA DAR ES SALAAM BAADA YA MKUTANO WA WAKUU WA NCHI WA NISHATI


******

Viongozi wa Afrika wameanza kuondoka jijini Dar es Salaam baada ya kushiriki kwa mafanikio katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere tarehe 27–28 Januari 2025.

Mkutano huo uliwakutanisha Wakuu wa Nchi 20 wa Afrika na Mwenyeji wao Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, maafisa waandamizi wa serikali, washirika wa maendeleo, na wadau wa sekta ya nishati, ambao walijadili mikakati ya kukabiliana na changamoto za nishati barani Afrika pamoja na kuchangamkia fursa zilizopo.

Mkutano huo, ulioandaliwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, umeweka historia kama hatua muhimu katika kuendeleza sekta ya nishati barani Afrika huku ukiwa umehudhuriwa kwa wingi na Wakuu wa Nchi wa Afrika.

Mkutano huo ulijadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa ya Afrika ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu, na endelevu kwa maendeleo ya bara zima la Afrika.

Mkutano huo umepitisha Azimio la Dar es Salaam, ambalo ni makubaliano muhimu yanayosisitiza dhamira ya pamoja ya viongozi wa Afrika kushughulikia mahitaji ya nishati bara Afrika.

Azimio hilo linaeleza hatua za kivitendo za kuongeza uwekezaji katika nishati mbadala, kuboresha biashara ya nishati katika kanda, na kuhakikisha upatikanaji wa nishati sawa kwa watu wote barani Afrika.

Baada ya kumalizika kwa mkutano huo, baadhi ya viongozi waliondoka nchini ambapo waliagwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na mawaziri na maafisa waandamizi wa serikali.

Miongoni mwa viongozi walioondoka ni Rais wa Kenya, Rais wa Djibouti, Rais wa Sierra Leone, Rais wa Botswana, Rais wa Mauritania, Rais wa Nigeria, Rais wa Guinea Bissau, Rais wa Ethiopia, Rais wa Madagascar, Rais wa Gabon, Rais wa Guinea Bissau, Makamu wa Rais wa Benin, Makamu wa Rais wa Gambia, mwakilishi wa Rais wa Algeria na wajumbe wa ngazi za juu ambao waliwakilisha serikali za Nchi zao







 

0/Post a Comment/Comments