Benki Kuu ya Tanzania imewataka wananchi wote kutumia Shilingi ya
Tanzania wakati wanapofanya miamala yao nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Januari 8, 2025, Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba
amesema ni kosa kununua, kuuza bidhaa na huduma hapa nchini kwa kutumia fedha
za kigeni.
Amesema kutumia fedha za kigeni kufanya miamala ya ndani ni kuhujumu uchumi
wetu na kunufaisha sera ya fedha ya nji za kigeni.
Gavana Tutuba amesema Benki Kuu itaendelea kusimamia utekelezaji wa Kifungu cha
26 cha Sheria ya Benki Kuu, 2006 kinachohimiza matumizi ya Shilingi katika
kufanya miamala hapa nchini ili kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni
yasiyokuwa ya lazima.
Gavana Tutuba ameyasema hayo wakati akizungumza na wakuu wa benki na taasisi za
fedha pamoja na waandishi wa habari wakati akitangaza uamuzi wa Kamati ya Sera
ya Fedha kwamba Riba ya Benki Kuu (CBR) kwa robo ya kwanza ya mwaka huu
itabakia kuwa asilimia 6, kama ilivyokuwa katika robo mwaka iliyopita.
Amesema uamuzi huo ambao ulifikiwa katika kikao cha Kamati hiyo iliyokutana
tarehe 7 Januari 2025 jijini Dar es Salaam umefikiwa kutokana na tathmini ya
mwenendo wa hali ya uchumi wa dunia na hapa nchini.
Kiwango hiki cha Riba ya Benki Kuu kinatumika wakati benki zinapofanya biashara
ya fedha kati yao.
Wakati huo huo, Gavana Tutuba amesema hadi hivi sasa, Benki Kuu imeshanunua
tani 2.5 za dhahabu ikiwa ni jitihada zake za kuongeza akiba yetu ya fedha za
kigeni.
Lengo ni kununua tani 6 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa fedha 2024/25
WANANCHI WAHIMIZWA KUTUMIA SHILINGI YA TANZANIA KUUZA NA KUNUNUA BIDHAA
*****
Post a Comment