WATUMISHI WA UMMA DAR ES SALAAM KUFANYIA KAZI NYUMBANI JANUARI 27 NA 28

****

Kufuatia ugeni mkubwa, baadhi ya barabara muhimu za Jiji la Dar es Salaam zitafungwa kama ilivyotangazwa na Jeshi la Polisi, na watumishi wa Umma wametakiwa kufanyia kazi zao nyumbani wakati wa Mkutano wa Wakuuwa Nchi za Afrika Kuhusu Nishati (Africa Energy Summit) utakaofanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 27 – 28 Januari, 2025

Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Moses Kusiluka amesema katika taarifa yake ya leo kwamba ili kuepuka usumbufu ambao unaweza kusababishwa na kufungwa kwa barabara hizo, Serikali inaelekeza kuwa tarehe 27 na 28 Januari, 2025 watumishi wa umma katika Mkoa wa Dar esSalaam wafanyie kazi nyumbani.

“Isipokuwa wale ambao mazingira yao ya kazi yanawataka kuwepo katika vituo vya kazi kama vile watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, sekta ya afya na sekta ya usafiri na usafirishaji”, amesema Dkt Kusiluka, huku akisistiza kwamba Benki hazitafungwa na biashara katika Soko la Kariakoo zitaendelea kufanyika. Hoteli na migahawa nayo haitafungwa.

“Waajiri katika sekta binafsi wanashauriwa kuruhusu watumishi wao katika Mkoa wa Dar es Salaam kufanyia kazi nyumbani au kuweka utaratibu ambao hautasababisha changamoto ya usafiri kutokana na kufungwa kwa barabara hizo” amesema Katibu Mkuu Kiongozi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan; Marais wa Nchi za Afrika 24; wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika 21; Wakuu wa Taasisi za Kimataifa sita (6) wakiwemo Rais wa Benki ya Dunia, Rais wa Benki ya Afrika na Rais wa Taasisi ya Rockefeller; na Washirika wa Maendeleo watano (5) watashiriki Mkutano huo.

 Aidha, jumla ya washiriki wengine 2,600 wa ndani na nje ya Tanzania wamejisajili kwa ajili ya Mkutano huo.


 

0/Post a Comment/Comments