****
Na Daniel Limbe,Chato
MKUU wa wilaya ya Chato mkoani Geita,Louis Bura,amewataka wazazi na walezi wilayani humo kuhakikisha watoto wenye umri wa kwenda shule wanapelekwa kupata haki yao ya msingi ya elimu pasipo visingizio vya aina yoyote.
Mbali na hilo,amewataka wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na elimu ya kidato cha kwanza mwaka 2025 kuripoti haraka kwenye shule walizopangiwa hata kama watakuwa na upungufu wa mahitaji ya shule.
Bura amesema ni maelekezo ya serikali kuwa wanafunzi wote waliochaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari waripoti hata kama watakuwa na uhaba wa vifaa vinavyohitajika shuleni kwa sababu serikali yao imeamua kutoa elimu bure kwa watoto wote wa kitanzania.
"Serikali ya awamu ya sita imeshatangaza kutoa elimu bure kuanzia msingi hadi sekondari ili kuwawezesha wananchi wote kupata elimu pasipo ubaguzi wa aina yoyote,hivyo hakuna sababu ya wazazi na walezi kushindwa kuwapeleka watoto wao kupata elimu inayo kusudiwa" amesema
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, mpaka kufikia Januari 23 takribani watoto 11,766 kati ya lengo la watoto 13,006 wamesha andikishwa kuanza elimu ya awali sawa na aslimia 90 ukilinganisha na aslimia 74 kwa mhula wa masomo wa 2024.
Kwa upande wa elimu ya msingi, takribani wanafunzi 16, 898 kati ya 16,687 wamepokelewa shuleni ikiwa ni aslimia 100.07 ukilinganisha na aslimia 113 za wanafunzi walio pokelewa mwaka jana licha ya kwamba bado mwitikio wa wazazi unaendelea kupeleka watoto wao.
Vile vile katika elimu ya sekondari takribani aslimia 58.9 wameripoti shuleni, huku wengine wakiwa hawajulikani walipo jambo lilioonekana kumkwaza mkuu wa wilaya hiyo na kulazimika kutoa kauli ya serikali kwa wazazi na walezi.
"Nitoe wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawahimiza watoto wao kuripoti shuleni kabla msako mkali haujaanza,tutawachukulia hatua kali wazazi na walezi wote watakao thibitika kukwamisha ndoto za watoto wao kwa kuwazuia kwenda shule kwa sababu zozote zile" amesema
"Aidha niwaombe walimu kutokuwa kikwazo kwa wanafunzi wote watakao ripoti shuleni wakiwa na uhaba wa vifaa vya shule ikiwemo sare,viatu na mahitaji wengine,wawapokee na masuala mengine yatafuata baadaye" amesema Bura.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mkuyuni, Goodluck Phinias,ameishukuru serikali kwa kuondoa sintofahamu kwa wazazi ambao walikuwa wakishindwa kupeleka watoto wao shule kutokana na kutokuwa na baadhi ya vifaa.
"Siye kama serikali ya kijiji cha Mkuyuni tunaungana na serikali kuu kuwahimiza wazazi kuwapeleka watoto shuleni ili wapate haki yao ya msingi kwa kuwa elimu ndiyo ufunguo wa maisha" amesema Goodluck.
Post a Comment