Waziri wa Ujenzi
Abdallah Ulega amesema atawapima mameneja wa Wakala wa barabara nchini
(TANROADS ), kwa uwezo wa kutatua changamoto
wakati wa dharura ili kuhakikisha barabara zote nchini zinapitika wakati
wote.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa wilaya za Handeni na Kilindi
alipokagua ujenzi wa barabara ya Handeni-Mafuleta KM 20 mkoani Tanga.
Amesema Meneja anayehakikisha barabara za mkoa wake
zinapitika vizuri bila msongamano na kutatua kero za watumiaji wa barabara
ndiye atahesabika kuwa meneja mzuri.
"Mh.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amenituma nipite kukagua miradi inayoendelea na iliyokwama ili niikwamue ",
amesema Waziri Ulega
Amemtaka Mkandarasi
Henan Highway Engineering Group (HEGO), anayejenga sehemu ya Handeni -Mafuleta kuendelea
kufanyakazi kwa bidii kwani ameshaanza kulipwa na ataendelea kulipwa ili
aendelee kuijenga barabara hiyo usiku na mchana kwa ubora uliokusudiwa.
"Kila mahala kwenye nchi hii kuna ujenzi unaendelea ,
Rais amedhamiria kuifungua nchi hii katika sekta zote ili kukuza uchumi wa
watu", amesisitiza Ulega.
Katika hatua nyingine Waziri Ulega amehimiza uharaka katika
zoezi la kubaini maeneo yenye milima na kona kali katika barabara ya
Segera-Chalinze ili zijengwe barabara wezeshi ili kupunguza msongamano na
ajali.
" Vifo na ulemavu vimeendelea kupoteza watu kutokana na
ajali za barabarani hivyo kamilisheni upembuzi yakinifu ili ujenzi katika
maèneo korofi uanze mara moja", amesema
Waziri Ulega.
Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Mohamed Besta amemhakikishia
Waziri Ulega kufanyiakazi maelekezo yake na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kulinda alama za barabarani.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni Albert Msando amesema barabara ya Handeni-Singida ni moyo wa uchumi wa wananchi wa Handeni na Kilindi kwani ni
muhimu katika shughuli za usafiri na usafirishaji hivyo kukamilika kwake kutachochea uchumi wa
wilaya za Handeni na kilindi na kuunganisha mkoa wa tanga na mikoa ya kati,
kanda ya ziwa.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilindi Mohamed Kumbi amemhakikishia
Waziri Ulega kuwa maendeleo yaliofanywa na Serikali katika Wilaya hiyo ni mengi
na wataendelea kuiunga mkono Serikali ili kufikia lengo.
Barabara ya Handeni-Mafuleta ni sehemu ya barabara kuu ya Handeni -Kiberashi -Singida yenye urefu wa KM 434.33 inayounganisha mkoa wa Tanga na mikoa ya Kati na kanda ya ziwa kukamilika kwake kutaleta tija kwa bandari ya Tanga.
Post a Comment