DC MPYA UBUNGO ASEMA ATASHUGHULIKIA MIRADI YA MAENDELEO KWA HARAKA


*****

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Lazaro Twange, amekutana na Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ili kujadili masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya wilaya hiyo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake baada ya kuteuliwa na Rais.

 Katika mkutano huo, Twange amehakikisha kuwa atashughulikia haraka masuala ya kijamii kama vile miundombinu ya barabara, upatikanaji wa maji, na masuala ya elimu.

Akizungumza katika mkutano huo, Twange alisema kuwa lengo lake kuu ni kupata taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na changamoto zilizopo katika maeneo mbalimbali ya wilaya, kuanzia ngazi ya kata. Alibainisha kuwa changamoto kubwa zinazotakiwa kushughulikiwa ni ujenzi na ukarabati wa barabara, masuala ya maji, na kuboresha elimu kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo, Juma Jaffari Nyaigesha, alieleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na halmashauri hiyo kukabiliana na changamoto za miundombinu, maji na elimu. Alisema kuwa fedha zimetolewa kwa kila kata ili kutatua changamoto hizo kwa haraka na ufanisi.

Madiwani, wakiwemo Ismail Malata (Diwani wa Kata ya Mbezi) na Ester Ndoha (Diwani wa Kata ya Goba), walimueleza Mkuu huyo wa Wilaya kuhusu changamoto kubwa zinazowakabili wananchi, ikiwemo ubovu wa barabara na uhaba wa maji safi katika maeneo yao.

Lazaro Twange anachukua nafasi ya Hassan Bomboko, ambaye amehamishiwa Wilaya ya Hai.











 

0/Post a Comment/Comments