TANZANIA MBIONI KUSAINI MKATABA WA ULINZI, USALAMA BAHARINI


...................

NA: Issah Mohamed –Dar es salaam.

EMAIL: issahmohamedtz@gmail.com

Serikali ya Tanzania kupitia wizara ya uchukuzi ipo mbioni kusaini mkataba wa makubaliano na Nchi zilizo ukanda wa Magharibi ikiwemo Kenya, Angola na Namibia utakaojielekeza katika kusimamia ulinzi na usalama Baharini.

Makubaliano hayo yamekusudia kupeana taarifa za usalama hatua ambayo imetajwa itapunguza athari mbalimbali ikiwemo uchafuzi wa mazingira, usafirishaji wa bidhaa haramu pamoja na madawa ya kulevya.

Hayo yamebainishwa Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa usalama na Mazingira wizara ya uchukuzi Bi Stella Katondo wakati akifunga warsha ya siku mbili iliyowakutanisha wadau wa sekta ya Bahari lengo likiwa ni kujadili mafanikio ya mradi wa kudhibiti uhalifu dhidi ya Meli.

‘’Swala la usafiri Baharini si la mpaka husimamiwa kimataifa lakini ili ufike huko kimataifa inabidi pia haya mataifa yanayohusiana kwa ukaribu yawe na makubaliano’’ Amesema Bi Katondo

Kwa upande wake Mkurugenzi wa usalama, ulinzi na utunzaji kutoka shirika la uwakala wa  meli Tanzania –TASAC, Bi Leticia Mutaki amesema Tanzania imeendelea kujipambanua katika ulinzi wa mazigira katika Bahari huku akisema kuwa mkutano huo umeongeza chachu ya kuboresha baadhi ya maeneo.

‘’Kwa Tanzania sasa hivi bado hatujawahi kuwa na tukio kubwa la uchafuzi licha ya kuwa na miradi mingi ikiendelea kwa mfano wa bomba la mafuta kutoka Uganda kwahiyo lazima tujiandae’’ Ameongeza Bi Mutaki.

Naye mmoja wa wanafunzi aliyeshiriki warsha hiyo ameipongeza serikali kupititia shirika la uwakala wa meli Tanzanzania –TASAC, kwa mafunzo hayo ambapo amesema yatamsaidia katika kufahamu ulinzi wa Bahari.

Mradi wa kudhibiti uhalifu dhidi ya meli pamoja na uchafuzi wa mazingira umeanza mwaka 2021 huku takwimu kuhusu mradi huo umeitaja Tanzania kuwa kinara katika utunzaji wa mazingira ukanda wa Bahari ya Hindi.

0/Post a Comment/Comments