*******
Wananchi wa Mtaa wa Saranga Mpakani, Wilaya ya Ubungo, wameiomba serikali kuwapatia huduma ya maji na kuondokana na changamoto hiyo iliyodumu kwa muda mrefu.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Lazaro Twange, wananchi hao wamelalamika kutokuwepo kwa huduma hiyo na kutegemea maji ya matanki, huku wakikabiliwa na changamoto ya kuamka alfajiri kwenda kutafuta maji. Wananchi hao wamesema kuwa ndoa zao ziko hatarini kutokana na muda mwingi kuutumia kutafuta maji.
Aidha, pamoja na changamoto ya maji, wananchi wa Mtaa wa Saranga wamemwomba DC kushugulikia changamoto ya ubovu wa barabara, ujenzi wa kituo cha polisi, na ujenzi wa zahanati.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Lazaro Twange, amewahakikishia wananchi wa Mtaa wa Saranga Mpakani kuwa ifikapo mwezi Machi 2025 wataanza kupata huduma ya maji na kuondokana na changamoto hiyo.
DC amemuagiza Meneja wa Dawasa Kanda ya Kinyerezi na uongozi wa mtaa kuzungukia nyumba ambazo zimejiunganishia maji bila kufuata utaratibu, jambo linalosababisha wananchi wengine kukosa huduma ya maji, ili marekebisho yafanyike. Hivyo, wananchi wengine wanaokosa huduma ya maji waweze kupata huduma hiyo. Kwa sasa, wananchi wanapata huduma ya maji kupitia matanki ambayo yanajazwa maji na Dawasa.
Kwa upande wake, Meneja wa Dawasa Kanda ya Kinyerezi, Crossman Makere, alieleza kuwa changamoto ya maji katika mtaa huo anaifahamu na imeanza kufanyiwa kazi. Zoezi la ulazaji wa mabomba linaendelea, ambapo mpaka sasa wameshafanikiwa kulaza mabomba kilomita tatu toka chanzo kilipo, na zimebakia kilomita tatu mpaka kufika eneo husika.
Post a Comment