*********
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekabidhi magari 12 kwa Maafisa wa Uthibiti Ubora wa Shule, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha mifumo ya usimamizi wa elimu nchini.
Magari haya yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.7 yamekabidhiwa kwa halmashauri 11 pamoja na ofisi za uratibu wa Mradi wa GPE-TSP waliofadhili ununuzi wa magari hayo.
Akizungumza hii leo Machi 14, 2025 Jijini Dar es salaam katika hafla ya makabidhiano Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa Wathibiti Ubora wa Shule wanafanya tathmini za kina kuhusu ubora wa elimu inayotolewa nchini, kufikia shule nyingi zaidi na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa walimu ili kuboresha matokeo ya wanafunzi.
Waziri Mkenda amesema magari hayo yatasaidia kurahisisha kazi za uthibiti ubora katika maeneo mbalimbali, huku akitaja halmashauri zilizonufaika kuwa ni Kibondo, Korogwe DC, Njombe TC, Tanganyika, Manyoni, Mbozi, Tunduma, Serengeti, Babati DC, Kahama Manispaa na Mafia.
Prof. Mkenda amebainisha kuwa mradi wa GPE umekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya uthibiti ubora wa shule ambapo awamu ya kwanza ilishuhudia ununuzi wa magari 38, na sasa idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia 50.
Post a Comment