********
Na Daniel Limbe,Chato
SIKU chache baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kutangaza kuanza kwa mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi nchini, Baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita wamemtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuanza mchakato wa kuomba kugawanywa jimbo jipya.
Kwa mujibu wa INEC mchakato huo unapaswa kufanyika kuanzia Februari 27,2025 hadi machi 26,2025.
Wakizungumza kwenye kikao cha robo ya tatu cha Baraza hilo,madiwani hao wamesema jimbo la Chato linapaswa kugawanywa ili kusogeza karibu zaidi huduma za jamii hatua itakayo saidia wananchi kutumia muda mwingi katika uzalishaji mali badala ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za kiserikali.
Diwani wa Kata ya Bwera,Josephat Manyenye, ndiye ameibua hoja hiyo kabla ya kuungwa mkono na madiwani wenzake kwa lengo la kuweka msisitizo wa maadhimio ya kikao hicho muhimu.
"Napendekeza Jimbo letu la Uchaguzi la Chato ligawanywe ili tupate Jimbo jipya kulingana na ongezeko la mahitaji ya kijamii na idadi ya watu tulionao, wilaya ya chato ina watu wanaozaliana kwa wingi kila mwaka na wanajituma sana katika kufanya kazi za kuwaletea maendeleo, hivyo upo umhimu mkubwa wa kuwasogezea huduma za msingi"amesema Manyenye.
Hoja hiyo ikamuibua Diwani wa Kata ya Buseresere,Godfrey Miti,ambaye amesema kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu kwenye kata ya Buseresere na Bwanga inatosha kabisa maeneo hayo kupatiwa Jimbo jipya la Uchaguzi,na kwamba ipo haja kubwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuanza mchakato wa kutuma mapendekezo hayo kwenye Tume huru ya taifa ya uchaguzi.
Vile vile Diwani wa Kata ya Muganza,Emmanue Mwita, amesisitiza mchakato huo kuanza haraka ili uweze kuwanufaisha wananchi wake ambao iwapo litatangazwa Jimbo jipya la Uchaguzi itasaidia sana jamii kupata maendeleo yanayokusudiwa na kupunguza migogoro isiyo kuwa ya lazima.
Hata hivyo,amegusia ugawanywaji wa baadhi ya kata kutokana na ukubwa wake ambapo baadhi ya kata hizo zimekuwa na maeneo makubwa ya kiutawala,hali inayosababisha baadhi ya wananchi kupata huduma za kijamii kwa umbali mrefu na wengine kutumia gharama kubwa.
Pamoja na mambo mengine, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Mandia Kihiyo, amewapongeza madiwani hao kwa kupendekeza uanzishwaji wa jimbo jipya la Uchaguzi,huku akiwasihi kuwa wavumilivu wakati taratibu za kuanza mchakato wa kukaa vikao vya uamuzi ukiandaliwa kulingana na ratiba iliyotolewa na INEC.
Amesema baada ya vikao vya kikanuni kukaa na kutathimini vigezo vinavyohitajika kutokana na maoni ya madiwani hao,Ofisi yake itahakikisha inapeleka haraka mapendekezo hayo ili kutoa mwanya kwa Tume huru ya taifa ya uchaguzi kuendelea na taratibu zake.
Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022,Jimbo la Chato lina jumla ya watu 584,963 huku wanaume wakiwa 286,138 na wanawake 298,825 huku jumla ya kaya zikiwa ni 110,156.
Mwisho.
Post a Comment